WAKULIMA wa miwa, wameshauriwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ushauri huo ulitolewa na wataalamu wa kilimo wa Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, walipozungumza na wakulima katika vijiji vinavyozalisha miwa ndani wilayani humo.
Ofisa Ugani wa Kijiji cha Kifinga, Kata ya Ruaha, Devotha Mng’andile, alisema wakulima wakizingatia utaalamu unaotolewa katika uzalishaji wa miwa, mnyororo wa thamani wa zao hilo utaongezeka na watakuza vipato.
“Tunachojivunia ni kuona maofisa ugani tuliopo vijijini tunawezeshwa kiutalaamu na wenzetu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI)-Kibaha, hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kuwafikishia wakulima maarifa mapya,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Tunachowaomba wakulima ni kuyafanyia kazi maarifa hayo.”
Alieleza wataalamu kutoka TARI- Kibaha wamewajengea uwezo wa kutosha wa kufahamu namna bora ya kuwahudumia wakulima wa miwa wilayani humo na tayari wameanza kuona mafanikio katika uzalishaji.
Ofisa Kilimo wa kijiji cha Lwemba, Kata ya Kidodi, Sarah Wolter, alisema kwa sasa pamoja na kutoa elimu kwa wakulima wa zamani, pia wameanza mchakato wa kutoa elimu kwa vijana ili washiriki katika kilimo cha miwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Kidodi AMCOS, Onesmo Mwakyambo, alisema kwa kushirikiana na maofisa Ugani na wataalamu kutoka TARI-Kibaha wanachama wake wamefaidika.
Mwakyambo alisema wamepata utaalamu wa uzalishaji miwa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya sayansi na teknolojia.
Kuhusu hatua ya usitishwaji wa vibali vya kuagiza sukari nje, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, alisema usitishwaji huo ni wa muda mrefu.
Aliweka wazi kuwa kusitishwa huko kumefanyika kwa mujibu wa sheria ya sukari namba 6 ya mwaka 2001, iliyofanyiwa mabadiliko mwaka jana.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, vibali vya uagizaji sukari nje ya nchi havitolewi, isipokuwa unapotokea upungufu na wazalishaji wanaopewa vibali vya kuagiza kwa muda.
Na MWANDISHI WETU



























