WAZAZI na walezi wanaolea watoto hasa wenye umri wa mwaka 0-8 wenye matatizo ya vichwa vikubwa na Mgongo wazi, wameiomba Serikali kuangalia kwa jicho la pekee gharama za kujiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya(NHIF) ambayo kwa sasa imekuwa kubwa na hivyo wao kujikuta wakiwa katika wakati mgumu kuhudumia watoto hao kwani hawana uwezo wa kulipia.
Wametoa ombi hilo walipokutana kujadili changamoto mpya wanazokabiliana nazo katika kuwalea watoto hao huku wakieleza gharama za kujiunga na mfuko wa bima ya afya imetoka Sh.50,400 hadi kufikia kati ya Sh.312000 hadi sh 360,000 kwa mwaka.
Hivyo gharama hizo ni mzigo mkubwa kwao hivyo ni vyema Serikali ikawashirikisha katika kuangalia njia rafiki itakayowarahishia kuwahudumia kimatibabu watoto hao.
Mkazi wa Barabara ya 14 Ngamiani jijini Tanga Asha Mohamed (31)amesema ni vema ifahamike kuwalea watoto hao ni changamoto kwa sababu wazazi hutumia muda wote kukaa nao hivyo kukosa nafasi ya kushiriki shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii na wengine wamesusiwa na waume zao.
“Huwezi hata kuchoma maandazi ukayatembeza mitaani kwa sababu huwezi kumuacha peke yake.Wengine hata kwenye misiba si rahisi kushiriki na maana yake tunajitenga na jamii na jamii nayo inatutenga. Ile Sh.50,400 ilikuwa ni mbinde kulipia je hii Sh. 312000 tutaipataje?”
Kwa upande wake Mayasa Selemani mkazi wa Genge wilayani Muheza amewaomba wahisani kujitokeza kuwapa msaada wa kuwalipia NHIF watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi ili kuwarahishia kupata matibabu wanapougua na kuhudhuria kliniki Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa wakati..
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi na Walezi wa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi (ASBHAT) Mkoa wa Tanga, Fatma kijavala ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kwa kuwapa kipaumbele watoto hao wanapougua.
Ameiomba Wizara ya afya kuweka utaratibu wa kuwapeleka Bombo wataalamu wa Kitengo cha MOI katika Hospitali ya Bombo angalau kila baada ya miezi sita ili kuwarahishia gharama za kuwafuata.
“Shukrani ziuendee uongozi wa Hospitali ya Bombo kwa kweli wanatupa kipaumbele,ukija na mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi wanamhudumia kwa haraka…
” Kama Wizara itakubali kuwaleta angalau mara mbili kwa mwaka wataalamu wa Moi ingetuondolea gharama za kusafiri kwenda Muhimbili na kukaa muda mrefu Dar es salaam kuwapeleka Muhimbili, ” alisema Fatma.
Kwa upande wake Mweka Hazina wa ASBHAT Taifa,Haji Naziru amesema mbali ya baadhi yao kutengwa na jamii,wazazi wenye watoto hao wanakabiliwa na hali duni kiuchumi.
“Kwenye orodha yetu kwa Mkoa wa Tanga tunao jumla ya watoto 122 wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi mbali ya Serikali hata wafadhili wenye kuguswa wangeweza kuwasaidia kuwalipia bima ya afya na gharama nyingine za kuwalea, ” amesema Haji.
Kwa upande wa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tanga, Mmassa Walele amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na wazazi hao na itawasilisha kwenye ngazi husika ombi la kurekebishiwa gharama za NHIF na kuletewa wataalamu kutoka Moi.
“Serikali inatambua changamoto za wazazi hao na ndiyo maana imewawekea mazingira rafiki katika hospitali ya Bombo, maombi waliyotoa ya NHIF na kuletewa wataalamu kutoka Moi angalau kila baada ya miezi sita nimeyapokea nitayafikisha kunakohusika” amesema Mmassa.