JUMLA ya warembo 20, wanatarajia kushiriki mashindano ya kumtafuta mlimbwende wa Ilala (Miss Ilala), yatakayofanyika Julai 31, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam baada ya uzinduzi wa mashindano hayo, Mratibu wa Miss Ilala, Lucas Lutainula, amesema moja changamoto walizokuwa nazo ni ukosefu wa wadhamini wa kusimamia mashindano hayo kwa mwaka huu.
Lutainula amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili kuwadhamini na kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.
“Mwaka jana tulishindwa kusimamia mashindano ya Miss Ilala kutokana na changamoto ya janga la corona, kazi nyingi zilisimama na hivyo hakukuwa na mashindano.
“Tunapitia changamoto mbalimbali kwa sasa na kwamba tunaomba wadau wajitokeze kutudhamini ili tufikie malengo tuliyojiwekea,” amesema Lutainula.
Mratibu huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi kutoa sapoti kwa vijana wao wanaoshiriki mashindano hayo ili kuwajengea uwezo wa kupata nafasi katika fainali za Miss Tanzania.
“Kumekuwa na dhana kwamba urembo ni uhuni, jambo ambalo halina ukweli ndani yake, tumeshaona warembo mbalimbali wakifanya vizuri na kuifanya sanaa hii kuwa ajira na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana vyema na Kampuni ya The Look, ambao ndio waratibu wa Miss Tanzania, ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.
Miss wa Ilala 2018, Linda Samson, amesisitiza wote watakaoshiriki katika mashindano hayo, kujipanga vyema ili kuleta ushindani na hatimaye wapatikane wawakilishi wazuri wa Miss Tanzania msimu huu.
Na AMINA KASHEBA