SERIKALI inatarajia kufanya tathmini na uhakiki kwa wananchi wa eneo la Kipunguni Jijini Dar es Salaam, waliopisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), ili walipwe fidia zao.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Segerea (CCM), Bonnah Kamoli.
Katika swali lake mbunge huyo alitaka kujua lini serikali itawapa barua wananchi wa Kipunguni ili wajue muda wa kufanyiwa uhakiki na lini watalipwa fidia zao.
Akijibu swali hilo, Mwakibete alisema serikali ilishaandika barua kwenda Jiji la Dar es Salaam tangu Aprili mwaka huu, na jiji watajibu kwenda kuwajulisha wananchi kwamba kazi hiyo ya tathmini inaanza rasmi ifikapo muda tajwa.
Kuhusu lini kazi hiyo itaanza, Mwakibete alisema wanatarajia kuanza kazi hiyo ya uhakiki Julai mwaka huu na kukamilika Septemba mwaka huu.
Awali, katika swali la msingi; Bonna alitaka kujua serikali inatoa kauli gani kuhusu wananchi wa Kipunguni ambao wamezuiwa kuendeleza maeneo yao tangu mwaka 1997, kwa lengo la kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
“Je, serikali bado ina mpango wa kuchukua maeneo,” alihoji mbunge huyo wa Segerea.
Akijibu swali hilo, Mwakibete alisema serikali ipo katika hatua za mwisho za kufanya uthamini mpya kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wote wa Kipunguni, waliopisha upanuzi wa uwanja huo wa JNIA.
“Nimhakikishie mheshimiwa mbunge na kuwaondoa hofu wananchi, zoezi la uthamini linatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu,” alisema Naibu Waziri huyo.
Na HAPPINESS MTWEVE DODOMA