WAMILIKI wa Hoteli mkoani Mbeya wamepongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha nchi kupata chanjo ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya UVIKO-19.
Wamesema hatua hiyo imewezesha kuondoa athari za zilizojitokeza kutokana na mlipuko huo ambapo sekta ya Utalii kwa ujumla ikiwemo hoteli na nyumba za kulala wageni ziliathirika kwa kukosa wageni.
Wamiliki hao walieleza hali hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na kundi la waandishi wa habari zaidi ya 30 wanaofanya ziara ya kutembelea na kutangaza vivutio vya utalii na Uwekezaji nchini ambapo mara hii wameangazia mkoa wa Mbeya.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usingilo ambao pia ni wamiliki wa Hoteli ya Usungilo iliyoko Kata ya Forest Mbeya mjini, Hotman Nyagawa, alisema ujio wa chanjo ya UVIKO-19 imewezesha sekta ya Utalii kuanza kurejea katika hali yake kawaida kama zamani.
“Mwaka 2020/21 sekta ya Utalii ikiwemo hoteli na nyumba za kulala wageni tuliathirika kwa kiasi kikubwa,hali ilikuwa mbaya hatukuwa tukipokea wageni pia sisi kwa sisi tulikuwa tunaogopana, tunamshukuru sana Rais, Samia kwa kuwezesha nchi kupata chanjo watu wamechanga na hivi sasa wanaendele na shughuli zao kama kawaida,”amesema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Hotel Desderia William Jima ameeleza kuwa wameweza kuchangia katika sekta ya Utalii ambapo wamekuajili Asilimia 98 ya Vijana kutoka mkoa wa Mbeya na nje ya mkoa wa Mbeya.
Kuhusu athari za UVIKO-19 amesema waliathirika kwa kiasi kikubwa baada ya mlipuko huo lakini kwa sasa hali imebadilika na wageni wameanza kuangia kama kawaida.
“Nawashauri watu wakachanje ili maisha yaweze kuendelea kwani ukichanja unakuwa umejikinga na mlipuko wa UVIKO-19, tusipuuze kuchanja maana ni kawaida yetu, japo kuchanja ni hiari,”amesema.
Hivi karibuni Rais Samia amezindua kampeni ya kuchanja kwa hiari inayoendeshwa nchi nzima.
Na Mwandishi Wetu,Mbeya



























