JESHI la Polisi mkoani Tanga, limewakamata watu wawili waliokuwa wakimiliki kiwanda cha kutengeneza silaha aina ya gobore kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi Tanga, SACP Safia Jongo, alisema walikamatwa katika Kijiji cha Mswaki kilichopo wilayani Kilindi, wakiwa na zana na vifaa mbalimbali vya kutengenezea silaha hizo.
Alisema pamoja na watu hao kukamatwa na vifaa hivyo, pia walikutwa na silaha aina ya gobore sita, vitako vya bunduki, mitutu na zana za kutengeneza bunduki hizo.
“Tumekamata bunduki sita, vitako, mitutu na zana za kutengenezea silaha, ni kiwanda cha kutengeneza silaha. Hii ni kila mwezi tunakamata kiwanda cha kutengeneza silaha wilaya za Handeni na Kilindi,” alisema.
Alisema katika msako wa kupambana na wahalifu wamewakamata wahalifu mbalimbali katika wilaya za mkoa huo.
Alitaja baadhi ya matukio ni pamoja na watu wanaoingiza wahamiaji haramu, waingizaji wa dawa za kulevya, kukutwa na mali za wizi, majangili wa nyara za serikali na waingizaji wa bidhaa za magendo.
Pia Kamanda Safia aliyemishiwa Tanga akitokea Tabora, alisema mtu mmoja alikamatwa wilayani Handeni akiwa na meno ya tembo mawili akisafirisha kwa pikipiki.
Mtu mwingine alikamatwa na nyara za serikali alikuwa mkazi wa Korogwe aliyekutwa na ngozi tatu za tandara na mwingine wa Kilindi alikutwa na kilo 120 za nyama ya twiga na kilo mbili za swala.
“Nyara zote hizo zilikuwa na thamani ya sh 80,498,910 na watuhumiwa watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika,” alisema.
Wakati huo huo, Jeshi hilo limewakamata watu watatu wilayani Kilindi wakiwa na noti bandia za sh. 2,140,000 wakiwa na lengo la kuzibadilisha ili wapate fedha halali.
Na Mashaka Mhando, Tanga



























