SERIKALI imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa hali ni shwari katika eneo la Ngorongoro na Loliondo, mkoani Arusha tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu.
Pia, imesema baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, navyo vimekuwa vikiripoti isivyo.
Serikali imesisitiza itaendelea kutekeleza haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi popote na kwamba, wananchi katika eneo tengefu la Ngorongoro, wataendelea kuhama kwa hiyari bila kushurutishwa na kutimiziwa yote waliyokubaliana.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam katika kikao kilichoitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali.
Katika kikao hicho, kilizihusisha Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Katiba na Sheria na Wakuu wa mikoa inayohusika na suala la Loliondo na Ngorongoro.
MAMBO YA NJE
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberatha Mulamula, alisema kumekuwa na upotoshaji mwingi juu ya kinachoendelea Loliondo na Ngorongoro.
“Kwamba wananchi wanaondolewa kwa nguvu na tunakiuka haki za binadamu. Kuna baadhi ya wanaharakati wanatembeza video kuwa watu wanauawa, wanapigwa mapanga, mambo ambayo si kweli,” alisema Waziri Balozi Mulamula.
Alieleza kuwa, wizara imeona umuhimu wa kukutana na wawakilishi hao wa jumuiya za kimataifa ili wataalamu waeleza bayana hatua zinazochukuliwa na serikali.
“Kinachoendelea Loliondo si kuhamisha watu. Hakuna mwananchi atakayehama. ila ni kuweka mipaka kati ya hifadhi na sehemu ya wananchi,” alifafanua.
Aliendelea kusisitiza kuwa mpango wa kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro ni shirikishi, umechukua miaka 20 hadi kufikia muafaka.
Balozi Mulamula alisema hadi kufikia jana, wananchi zaidi ya 200 walikubali kuhama kwa hiyari kwenda eneo lililoandaliwa na serikali, Handeni mkoani Tanga.
“Taarifa waliyopewa mabalozi, itaondoa sintofahamu iliyopo, tunawaomba waandishi wa habari msaidie kueleza ukweli. Hali iko shwari, bahati mbaya aliuawa askari polisi aliyekuwa akisimamia zoezi hilo,” alibainisha waziri huyo.
Alisema jambo la kushangaza, licha ya askari huyo kuuawa, hakuna chombo chochote cha habari cha kimataifa kilichoeleza juu ya tukio hilo.
“Katiba yetu inatambua usawa wa kila mmoja. Haki ya kila mmoja kuishi popote nchini. Inatambua haki za maliasili zetu. Mabalozi wamefurahishwa kwa kupata taarifa ambazo hazipatikani katika mitandao,” alisema Waziri Mulamula.
Pia, alisema vyombo vya kimataifa, Umoja wa Mataifa (UN), vimekuwa vikitafuta majibu ya kinachoendelea Loliondo na Ngorongoro, hivyo anaamini kupitia mkutano huo, jumuiya ya kimataifa imepata uelewa halisi.
WIZARA YA MALIASILI
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja, alitumia kikao hicho kukemea kuchafuliwa kwa wawekezaji na uzushi unaoenezwa kuhusu serikali ya awamu ya sita.
“Kuna malalamiko na minong’ono mbalimbali inayosema kuna mwarabu amepewa eneo la Loliondo. Nataka niwaambie Watanzania, wawekezaji hawajaanza leo kuwekeza katika hifadhi ya Lolindo.
“Kampuni ya OBC ipo hapo tangu awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi (Rais Mstaafu), mwekezaji alipewa kile kitalu, Kampuni ya OBC.
“Wala siyo mwindaji kama wengine wanavyosema anaiba wanyama wetu. Si kweli, hata kama wakichunguza wataona,” alisema naibu waziri huyo.
Alifafanua: “Inaonekana kama vile mwekezaji huyo (OBC) amekuja wakati wa serikali ya awamu ya sita. Si kweli, nataka hili wananchi walifahamu, vyombo vya habari vinapotosha. Mwekezaji huyu yupo zaidi ya miaka 30, yuko pale na anamiliki vitalu.
“Wengine wanasema serikali hii ya awamu ya sita ndiyo imekuja na huo utaratibu, jamani tena nataka niwahakikishie, zoezi hili lilikuwa litekelezwe na Hayati Dk. John Magufuli, Mama (Rais Samia Suluhu Hassan), anatekeleza kile ambacho amekikuta mezani tu.”
Naibu waziri huyo aliongeza: “Harakati zimeanza mwaka 2008 wakati wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, imekuja hadi 2013, maazimio yako mezani, hata mimi sikuwepo, leo tunatekeleza yale ambayo yaliazimiwa na Baraza la Mawaziri.”
Naibu Waziri Mary alifafanua kuwa, kila baada ya muda, serikali hutangaza uwekezaji katika vitalu hivyo na kwamba, hivi karibuni vilitangazwa na mwekezaji huyo akaomba kama wengine, akashinda mchakato.
UFAFANUZI ZAIDI
Naibu waziri huyo alisema katika eneo hilo, kumekuwa na upotoshaji mkubwa huku wengi wakiamini ardhi ya Loliondo ni ya watu wa kabila la Masai.
“Kabla ya kuanzishwa hifadhi hii, katika eneo hilo kulikuwa kuna kabila la Wahadzabe, baadae likaja kabila la Watoga, kisha Wamasai,” alifafanua.
Alisema wakati eneo ilipo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, lilipoonekana linafaa kuhifadhiwa, Wamasai waliokuwa wanaishi humo, walihamishiwa Ngorogoro na kuwekwa sheria katika hifadhi hiyo.
“Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kuwa, hilo ni eneo la Masai. Si kweli, tukirudi katika historia wenye kudai ardhi yao ni Wahadzabe,” alisema.
Aliongeza kuwa, mwingiliano wa wanyamapori na binadamu, unafanya uhifadhi kushindikana, lakini serikali imetumia busara kuwaondoa wananchi kwa hiyari.
“Unapofika Ngorongoro, unakutana na makundi makubwa ya ng’ombe, watoto hawaendi shule, wanakuwa ombaomba huo nao ni ukiukwaji wa haki za binadamu,” alieleza naibu waziri huyo.
Alisema kuwa, ufugaji wa ng’ombe unaoendelea Ngorongoro na Loliondo, kwa asilimia kubwa unatokea nchi jirani.
“Lolindo iko mpakani mwa Tanzania na Kenya, kumekuwa na mwingiliano wa shughuli za kibinadamu, inasemakana kwa asilimia kubwa, mifugo inayoingia nchini, mingi ni ya wageni kuliko wenyeji,” alisema.
Aliongeza: “Mifugo inaingia lakini, ukiwaangalia wenye mifugo wenyewe sisi serikali ndiyo tunaowalisha, tumekuwa tukipeleka chakula Ngorongoro, wananchi wanakutwa na janga la njaa, lakini unamkuta huyo mwananchi anayemiliki mifugo zaidi ya 1,000 ni ombaomba, ni masikini hana chakula ndani.
“Kwa hiyo, tulifanya utafiti, tukagundua mifugo inazidi kuongezeka, Tanzania imekuwa shamba la bibi, watu wamekuwa wakileta mifugo yao kunenepesha na haiuzwi Tanzania.
“Bora hata tungekuwa tunauza Tanzania tungepata fedha za kigeni. Lakini ile mifugo ikishanenepa, inasafirishwa kwenda nchi za wenzetu, wanafanya biashara.
“Kwa hiyo sisi hakuna chochote tunachofaidika nacho, tulipofanya hii sensa, tukagundua mifugo iliyoko huko siyo ya wananchi, ushahidi umeonekana, tumehamisha watu kaya 20, ng’ombe walioenda huko (Tanga), hata laki moja hawafiki.”
Alisema jamii inatakiwa ijiulize, makundi makubwa ya mifugo yaliyokuwa yanaonekana Ngorongoro awali, yamekwenda wapi.
“Tunachotaka kusema ni kwamba, mle ndani uhifadhi umeathirika sana, angalau wangekuwa wanafaidika wale wenyeji, lakini hawanufaiki. Wanaonufaika ni wanaokuja kunenepesha mifugo yao na kuondoka.
“Ndiyo maana tukasema kama ufugaji upo kweli na mifugo ni ya kwetu, tuna maeneo makubwa ambayo tunaweza kuyatoa kwa wafugaji wetu,” alisisitiza naibu waziri.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, alisema katiba inaelekeza wazi kuwa, ardhi ni mali ya serikali.
“Kinachofanyika kule ni serikali kutoa ardhi kwa wananchi, siyo kuwapora. Serikali ndiyo mmiliki wa ardhi,” alisema Dk. Ndumbaro.
Waziri huyo, alisema hakuna ardhi inayomilikiwa na kabila hapa nchini.
Na CHRISTOPHER LISSA