WANAFUNZI wawili wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhemeli, iliyopo Kijiji cha Uhemeli, Kata ya Ndala, Tarafa ya Puge, Wilayani Nzega, mkoani Tabora, wameuawa kwa kukatwa shingo na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi, Mkoani humo, Kamishna msaidizi wa polisi Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuwataja waliouawa kuwa ni Richard Gibe (12) na Wamba Gibe (10), wakazi wa Kijiji cha Uhemeli.
Amesema watoto hao waliuawa walipokuwa wakichunga Ng’ombe, ambapo inadaiwa walirubuniwa na mtuhumiwa, kabla ya kutekeleza mauaji hayo na kufukia miili katika shimo la takataka nje ya nyumba ya bibi yake.
Aliongeza kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye jina lake limehifadhiwa alipora ng’ombe saba wenye thamani ya sh. milioni 4.9 waliokuwa wakichungwa na watoto hao.
Kamanda Safia alibainisha kuwa baada ya kupata taarifa za tukio hilo polisi walifanya uchunguzi wa kina na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne ambao baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika na mauaji hayo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kupitia operesheni zinazofanywa na askari wa jeshi hilo ili kukomesha vitendo hivyo.
Pia, amewataka wale wote wanaomiliki silaha kinyume na utaratibu kuzisalimisha mara moja, kabla hawajakamatwa.
Na ALLAN KITWE, TABORA



























