MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amesema hadi sasa wananchi 1,000, wamewasilisha maombi ya kupata chanjo ya corona mkoani hapa na kusisitiza kuwa, wengine zaidi wanaendelea kujitokeza kwa hiari kupata chanjo hiyo.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Sinodi wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Mtaka alisema tayari maelekezo mazuri kuhusu chanjo hiyo yameshatolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo wananchi wajitokeze kwa hiyari kupata chanjo hiyo.
“Rais ameshasema yeye ni mama wa familia, ni bibi wa familia, anabeba dhamana ya nchi kama Rais. Kama lingekuwa jambo baya, asingeingia katika suala hilo na bahati nzuri jambo hili lipo huru.
“Niwaombe mchanje na muepukane na siasa ya chanjo, uhai wako siyo mali ya kanisa, uhai wako siyo mali ya msikiti, wewe utakufa msikiti utakuwepo, kanisa litakuwepo,” alieleza.
Aliongeza kuwa chanjo hiyo siyo ya kwanza, kwani wananchi walishapatiwa chanjo ya surua na polio, hivyo wasikubali upotoshaji.
Mtaka alisema viongozi wa kanisa hilo wanakaribishwa kupata chanjo na kusisitiza kuwa, maelekezo zaidi yatatolewa.
Vilevile, Mtaka alieleza dhamira ya mkoa kufanya usajili wa wakulima kujua wapi walipo, wanataka kulima zao gani na ukubwa wa eneo husika.
“Lengo letu hapa ni kuboresha kilimo chetu na baadae tupate zana bora kama trekta. Kiu yangu ni kuwa na mkoa, ambao faida ya makao makuu inaonekana kwa kuanzia kwa wananchi,”alisema.
Aliwahimiza wananchi kujenga tabia ya kupanda miti ya kivuli na matunda, kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kuenzi kampeni ya utunzaji wa mazingira, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
“Sasa hivi msimu wa mvua unakuja, siyo vibaya kanisa mkaandaa kila mtu miche 10, ya michungwa, embe au tunda lingine, tukapanda katika maeneo yetu ya kanisa na hata nyumbani, ninatamani kuiona Dodoma ikiwa ya kijani kwa kila kaya kupanda miti.
“Katika kuhakikisha kila mtu anashiriki utunzaji wa mazingira, kutakuwa na wiki maalumu ya kuchimba mashimo, wiki ya kuweka mbolea na wiki ya kupanda miti, nataka kila mmoja atumie mvua za mwaka huu kupanda miti,” alisisitiza.
Awali,akizungumza katika mkutano huo, Askofu wa Dayosisi ya Kati ya Kanisa la Anglikana (DCT), Dk. Dickson Chilongani, alisema binafsi anaamini katika chanjo.
“Mimi naamini katika chanjo. Ombi langu ni moja, serikali itoe elimu zaidi kwa wananchi juu ya chanjo, kuondokana na fikra potofu, ambazo wanaambiwa na watu.
“Huko vijijini, watu waelimishwe kwa nini mara ya kwanza waliambiwa wasichanje na sasa hivi wanaambiwa wachanje, serikali iwaelimishe ili wajue,” alisema.
Na SAKINA ABDULMASOUD, DODOMA



























