WATU wawili wakazi wa Arusha, wamekamatwa na Polisi katika Kituo cha mabasi cha wilaya ya Sikonge, Tabora kwa tuhuma za kukutwa na madini feki waliyokuwa wakiwauzia wananchi.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, aliwataja Mariam Said, akiwa na dereva wake, David George wakiwa na madini hayo, inadaiwa waliyatumia kumtapeli mkazi wa Kijiji cha Usunga wilayani humo aliyefahamika kwa jina moja la Edward.
Alidai watuhumiwa walikamatwa baada ya kudaiwa kumtapeli mkazi huyo sh. 340,000, baada ya kukaguliwa, walikutwa na kadi tano za benki tofauti tatu za NMB, Benki ya Posta na CRDB.
Vitu vinginevyo walivyokutwa navyo ni simu nne aina ya Iphone 6s plus, Tecno Spark 5 Air, Infinix hot 10 na Samsung zinazodhaniwa kuwa za wizi.
Abwao alisema kuwa, madini hayo yamekamatwa kutokana na juhudi za Polisi kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuzuia na kupambana dhidi ya uhalifu.
Aidha, aliongeza kuwa, katika kukabiliana na matukio ya uhalifu, mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, ujambazi na uvunjaji mkoani humo, jeshi hilo limeendelea kufanya operesheni katika wilaya zote.
Alitaja mafanikio ya oparesheni hiyo kwa mwezi huu kukamatwa watu wawili, Khamis Baruti na Mohamed Shabani, wakazi wa Izimbili wilayani Uyui baada ya kukutwa na silaha aina ya gobore isiyokuwa na namba za usajili iliyokuwa ikitumika katika uwindaji haramu.
Aidha, walikamata silaha mbili aina gobore zilizosalimishwa na watu wasiojulikana katika Kata za Kipanga na Mole (Usanganya) wilayani Sikonge na silaha nyingine ilisalimishwa na mkazi wa Mibono, John Matuzya katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kiloleni akidai anatii sheria bila shuruti.
Kamanda alitoa wito kwa wananchi wanazomiliki silaha kinyume na utaratibu kuendelea kuzisalimisha ndani ya kipindi hiki cha msamaha, vinginevyo watakamatwa, aliitaka jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Na ALLAN KITWE, TABORA



























