WIMBI la tatu la ugonjwa wa virusi vya corona (uviko-19) linaloikabili dunia, imegeuka kuwa fursa kwa idadi kubwa ya wanawake wengi nchini.
Hatua inatokana na kundi hilo kujikita katika biashara ya bidhaa mbalimbali zinazotumiwa katika afua ya kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo barakoa.
Wakizungumza Dar es Salaam, baadhi ya wanawake wanasema fursa wanayoitumia wakati wa ugonjwa huo, imewaokoa katika wimbi la manyanyaso kutoka kwa wenza wao, na kuwawezesha kumudu maisha ya familia na kujenga heshima.
Katika mazungumzo yao na UhuruOnline, wanawake hao wanasema biashara ya bidhaa za kujikinga na uviko-19, imekuwa mkombozi wa kile walichokiita dharau, kebehi na mateso dhidi ya wenza wao, huku baadhi yao wakikiri kunusurika kuachika katika ndoa zao.
Baadhi yao wanasema awali, wenza wao walikuwa wakiwaona ni mzigo ndani ya nyumba kwa kile walichoamini hawakuwa na mchango katika ustawi wa uchumi hasa linapokuja suala la matumizi ya chakula, kusomesha watoto na mambo mengine ya msingi ya kifamilia.
Shukurani Msemo ni mfanyabiashara wa barakoa katika kituo cha mabasi yaendayo Haraka (DART) cha Tiptop-Manzase, anasema biashara hiyo imemwezesha kuhudumia familia yake yenye mume na watoto watatu.
Shukurani anasema kabla ya biashara ya barakoa, aliishi maisha ya shida na mumewe ambaye, alikuwa akimuachia sh. 2,000 kwa siku kwa matumizi ya nyumbani, fedha ambayo haikutosha hata kwa mlo mmoja wa siku.
Anasema fedha alizokuwa akiachiwa kilitokana na uhalisia wa kipato cha mumewe kwa kuwa katika shughuli zake alizokuwa akifanya asingeweza kumwachia zaidi ya kiasi hicho.
“Wakati huo mimi sikuwa na shughuli ya kufanya, mume wangu ndiye aliyekuwa anakwenda katika mihangaiko ya kila siku lakini kipato chake hakikutosheleza huduma za familia hii yenye watu watano, nilijaribu kumwambia anisaidie mtaji nitafute biashara lakini ilishindikana,” anasema.
Shukurani anasema alipata wazo la kuuza barakoa, lakini hakuwa na mtaji, hivyo ilimlazimu kuweka akiba ya sh. 500 kila siku kati ya sh. 2,000 alizokuwa akiachiwa kwa matumizi ya chakula ya nyumbani. Hivyo alitumia sh. 1,500 kila siku pasipo mumewe kujua.
Mjasiriamali huyo anasema kuwa baada ya kuhifadhi kiasi hicho cha fedha alifikisha sh. 10,000 zilizotosha kununua boksi moja la barakoa na kuanza biashara hiyo.
“Kuna rafiki yangu alinishauri kuhusu biashara ya barakoa, wakati huo yeye alikuwa anafanya biashara hiyo, ndipo nilipopata wazo la kuhifadhi fedha na baada ya mwezi mmoja ilifika sh. 10,000 akanipeleka kununua boksi moja na nikaanza biashara,” anasema.
Shukurani anasema baada ya kuanza biashara hiyo, wamekuwa wakipata milo mitatu kwa siku na yeye akiwa ni tegemeo kubwa ndani ya familia.
“Kuna wakati mume wangu haniachii fedha za matumizi ya siku, lakini anakuta nimepika na wanangu wanakula vizuri, wote tuna furaha. Kabla ya biashara hii alikuwa akiniita majina yasiyofaa lakini sasa naona upendo na heshima imeongezeka,”anasema.
Shukurani anadokeza kwa siku anapata kati ya sh. 15,000 hadi 20,000 kulingana na biashara kwa siku husika na amejipanga kuanzisha biashara nyingine ili kuongeza kipato katika familia.
Kauli ya Shukurani inaungwa mkono na Naima Sauli, anayefanya biashara ya barakoa jijini, ambaye anasema huangalia fursa ya maeneo yenye mikusanyiko ya watu yanayolazimisha uvaaji wa barakoa akitoa mfano wa hospitali na maeneo mengine muhimu.
Anasema biashara ya barakoa anafanya zaidi katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Muhimbili na Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati matukio ya michezo.
“Kwa mfano siku ya Tamasha la Yanga nilikwenda na barakoa zangu nilizotengeneza kwa fundi nimeziweka nembo ya Yanga, nilirudi nyumbani na sh. 100,000 kila barakoa niliiuza sh. 2,000,” anasema.
Anasema biashara hiyo imemfanya kuona umuhimu wa kutumia fursa katika jambo lolote linalotokea duniani na anasisitiza bila barakoa asingepata mafanikio aliyonayo.
“Sina mume lakini nina watoto watatu, kabla nilifanya biashara ya mamalishe, lakini uuzaji wa barakoa una faida kuliko mamalishe, kwa sasa nimeamua kuacha na kujikita katika barakoa,” anasema.
Anasema kupitia biashara ya barakoa, anamudu gharama za nauli ya wanawe kwenda na kurudi shuleni, kuihudumia familia, kulipa kodi ya nyumba mambo ambayo alipokuwa mamalishe alishindwa kuyatimiza kwa wakati.
“Nilipokuwa mamalishe kuna wakati nilibaki na nauli yangu, maana yake nikiwapa watoto waende shule mimi nabaki nyumbani au nikienda nayo mimi kazini watoto hawaendi shule, maisha yalikuwa magumu sana,” anasema.
Wakati Naima akitoa maelezo hayo, Lucy Koja, anayeuza barakoa katika soko la Mabibo, anasema ingawa biashara hiyo imedorora sokoni hapo kutokana na mwamko mdogo wa watu kuvaa barakoa, lakini imetofautisha maisha yake ya awali na sasa.
“Zamani nilikuwa nauza makopo nayaokota nakwenda kupima na kuuza, kwanza nilionekana chizi maana ile shughuli unatafsiriwa vibaya, pili niliishia kupata hela ya kula mlo mmoja wa siku. Lakini kwa sasa nimemfuata mwanangu kijijini naishi naye kuwa kuna nina uhakika wa kipato,” anasema.
Kwa upande wake, Nawale Singano anayefanya biashara katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), anasema barakoa zina historia kubwa katika maisha ya ndoa.
Anasema kabla ya kuanza biashara hiyo alinusurika kuachika, kwani ulifika wakati mumewe alikosa fedha za kuhudumia familia na kumtaka arudi kwa wazazi wake mkoani Songwe.
Nawale anasema mumewe alifikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa asingeweza kuihudumia familia kutokana na kipato kidogo, hivyo alitaka abaki mwenyewe.
“Kila biashara niliyofikiria kufanya kumsaidia mume wangu mtaji wake ulianzia sh. 100,000 na zaidi, hivyo sikuwa na uwezo wa kupata, lakini nilipoona wanawake wengine barabarani wanauza barakoa niliuliza nikaambiwa boksi moja ni sh. 10,000 nilitafuta nilipopata nikaanza biashara na sasa mambo mazuri
“Mwenzangu akitoka nami nikitoka tukirudi tunakusanya kiasi kikubwa, hivi ninavyokwambia tuna akiba tunataka kufungua duka la bidhaa mbalimbali, uviko-19 imekuja na fursa kubwa hasa kwetu wanawake.
“Tulikuwa tukigombana na mume wangu kila siku akinitaka nirudi nyumbani, lakini siku hizi upendo umeongezeka, tunazungumza vizuri na mipango yetu ni mizuri, nawashauri wanawake watumie fursa zilizoko kujipatia kipato,” anasema Nawale.
JUMA ISSIHAKA NA IBRAHIM HUSSEIN (UDSM)