WAKAZI wanne wa Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka mawili, likiwemo la wizi wa sh. milioni 480.5 mali ya Msikiti wa Street Sanatan Dharma Sabha.
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya ambao ni Akshary Motichand (22), Vasant Solanki (73), Ramesh Shah(62) na Shailesh Chauda(48).
Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Yusuph Aboud, alidai katika shtaka la kwanza, washitakiwa hao kati ya Januari mwaka 2016, walikula njama kwa nia ya kutenda kosa.
Aboud alidai katika shtaka la pili, washitakiwa hao katika tarehe hiyo na mwaka huo, wakiwa maeneo ya Dar es Salaam, waliiba sh. 480,509,088, mali ya Msikiti wa Street Sanatan Dharma Sabha.
Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa.
Hakimu Isaya alitaja masharti ya dhamana kwa washitakiwa hao ambao aliwataka kuwa na wadhamini wawili, kati yao awe na hati ya mali yenye thamani ya sh. milioni 60 isiyohamishika au fedha taslimu kiasi hicho.
Hati hizo zililetwa mahakamani na baada ya kufikishwa zilipelekwa kuhakikiwa kabla ya kupata dhamana.
Na SYLVIA SEBASTIAN





























