WATALII 550 kutoka Israel wanatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete amesema watalii hao, watatembelea hifadhi za taifa zilizoko Kaskazini mwa Tanzania pamoja na eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
“Kundi la kwanza la watalii 150, litawasili kwa ndege binafsi kutoka nchini Israel katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro saa 11 alfajiri kesho (leo)” alisema Shelutete katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
Alisema kundi la pili la watalii hao litawasili Agosti 9, mwaka huu, likiwa na watalii 200 na kundi la tatu litawasili Agosti 16, mwaka huu na kwamba, makundi yote yatashukia KIA.
Shelutete alisema ujio wa watalii hao unatokana na juhudi za utangazaji wa utalii katika soko la sekta hiyo inayokuwa kwa kasi nchini humo.
Alitaja sababu nyingine iliyoongeza idadi ya watalii ni jitihada za serikali ya awamu ya sita kukabiliana na ugonjwa wa uviko 19.
“Ongezeko hili pia linatoka na kuzingatia kanuni na miongozo inayotolewa na Shirikaa la Afya Duniani (WHO), ikiwemo utolewaji wa chanjo ya ugonjwa wa uviko 19,” alisema.
Alitaja sababu nyingine ni serikali kufungua ubalozi wake nchini Israel, hali ambayo imeleta hamasa kubwa kwa wananchi nchini humo kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na ubalozi huo.
Alisema kwa kipindi cha mwaka jana, Tanzania ilipokea watalii zaidi ya 1,000 kutoka Israel, ambao walipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Watalii hao wanatarajiwa kupokelewa na viongozi mbalimbali wa serikali, sambamba na kufanyika kwa hafla fupi ya kuwapokea itakayofanyika uwanjani hapo.
Na LILIAN JOEL, Arusha



























