RAIS Samia Suluhu Hassan,amesema Mkoa wa Arusha umefurika watalii na kusisitiza amani na utulivu maeneo yote ya nchi, ili watalii hao wawe mabalozi wazuri wa Tanzania watakaporejea kwao.
Amesema Tanzania imejipambanua vizuri duniani katika eneo la amani, utajiri wa vivutio vya utalii na uwepo wa watu wakarimu walio tayari muda wote kupokea vizuri wageni.
Rais Samia amesema hayo, jijini Dar es Salaam, wakati akihitimisha Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 25 ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).
“Arusha sasa watalii ni wengi sana, hivyo tudumishe amani na utulivu, ili watalii hawa wanaoendelea kuja nchini, Arusha, Zanzibar na maeneo mengine waondoke na kumbukumbu nzuri ya kuwashawishi wengine waje,” alisema.
Kadhalika, Rais Samia amesema serikali inaendelea kuitangaza nchi na fursa zake za utalii na uwekezaji, hivyo wajasiriamali wa makundi yote hususan wanawake, wajizatiti kunufaika na hatua hiyo.
Amesema wajasiriamali wakiwemo wanufaika wa EOTF, waamue kuzalisha bidhaa zenye ubora wa juu ambao utazipa bidhaa husika kibali cha kuliteka soko la kimataifa dhidi ya bidhaa zinazotengenezwa maeneo mengine duniani.
Rais Samia ameutaka uongozi wa EOTF, kuwajengea uwezo wa elimu ya biashara wanufaika wake kwa kushirikiana na mamlaka na taasisi nyingine akizitaja Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Amesema awali alipopata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho kama sehemu ya sherehe za EOTF, alifurahishwa na uwepo wa idadi kubwa ya wajasiriamali waliofanikiwa kuzirasimisha biashara bidhaa zao ili kuzinasa fursa zinazotokana na matokeo ya filamu ya Tanzania The Royal Tour.
SIRI YAKE NA EOTF
Rais Samia katika hotuba yake, alisema EOTF yenye miaka 25 sasa, imemuingiza katika duru za siasa kupitia kwa mwasisi wake Mama Anna Mkapa, ambaye ni mke wa Hayati Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Alisema katika moja ya matukio ya kutembelea vikundi vya vijana, Chamazi wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam, aliachwa na msafara wa magari uliokuwa ukienda eneo la tukio.
“Nilikuwa nimezubaa, nikaachwa na magari, sasa Mama (Anna Mkapa) akaniona akiwa ndani ya gari lake, akaniita wewe ‘Mpemba’ mbona umezubaa hapo?”…nikamjibu nimeachwa na gari, akaniambia njoo upande humu twende.
“Tukiwa mule ndani, alianza kuniambia: Samia, nimekuangalia tangu umekuja hapa EOTF, wewe ni mwanasiasa mzuri, uchaguzi ujao hebu jaribu…nikamjibu sijui watu wanaingiaje; akaniambia wewe ulizauliza tu kule kwenu Pemba utaelekezwa,” alisimulia.
Rais Samia aliendelea: “Nilikwenda nikafuatilia na baada ya kuona maswali mengi ya kero za wananchi, yanayohitaji majibu Baraza la Wawakilishi, nikashawishika kuingia.”
“Nikachaguliwa mjumbe wa Baraza, baadaye waziri, nilipogombea tena, waziri, halafu waziri tena baadaye mgombea mwenza wa urais, hadi sasa lakini nguvu ya kuingia ni maneno ya Mama Mkapa,” alisema.
Alisema Mama Mkapa kupitia taasisi yake kwa miaka 25, amefanya kazi kubwa ya kulea maelfu ya wanawake na kuwatoa katika mazingira ya chini hadi kuwa watu muhimu katika taifa.
Rais Samia alitumia fursa hiyo kumpongeza na kuitaka taasisi hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo yanagusa moja kwa moja utekelezaji wa sera ya taifa ya maendeleo ya jamii ya mwaka 1996.
“Serikali tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hii na zingine zinazofanya kazi muhimu ya kuisaidia serikali kugusa maisha ya wanawake na makundi mengine maalumu kujikimu kimaisha,” alisema.
Rais Samia alieleza serikali ya awamu ya sita licha ya kusimamia upatikanaji wa mahitaji muhimu ya jamii, ikiwemo elimu bora, maji safi na salama, huduma bora za afya na miundombinu ya barabara, bado jiografia ya nchi ni kubwa na mahitaji ni mengi, hivyo upo umuhimu wa taasisi binafsi kushirikiana na serikali kikamilifu.
AMPA MAAGIZO MAKALLA
Katika hatua nyingine, Rais Samia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, kuielekeza Manispaa ya Temeke kutenga fedha za asilimia 10, kwa ajili ya kununua pikipiki ya matairi matatu maarufu bajaji, itakayotumiwa na wasichana wanufaika wa EOTF, ambao baada ya kuhitimu elimu ya juu na kukosa ajira, waliamua kuelimisha umma juu ya umuhimu wa lishe.
“Nilipokuwa napitia mabanda ya maonyesho kule nje, nilikutana na binti mmoja ni mhitimu wa chuo, baada ya kukosa ajira akaamua kutoa elimu ya lishe mahospitalini akiwa na wenzake, changamoto yao aliyonieleza ni usafiri.
“…nimemuuliza bajaji itatosha? Akasema ndiyo na kushukuru mpaka akapiga magoti, sasa RC (Makalla) wasiliana na Halmashauri ya Temeke, kutoka katika zile asilimia 10, watafute fedha wanunue bajaji kwa ajili ya kikundi hiki,” alisema Rais Samia.
Vilevile, Rais Samia alimuagiza mkuu huyo wa mkoa, kutafuta eneo la ujenzi wa Kituo cha Biashara cha Wanawake, ambacho Mama Anna Mkapa alimweleza awali, kwamba EOTF inakusudia kukijenga kwa ajili ya kumwinua zaidi mwanamke wa Tanzania kiuchumi kutokana na fursa nyingi zilizopo sasa.
MAMA ANNA MKAPA
Akizungumza awali, Mwenyekiti wa EOTF, Mama Anna Mkapa, alisema taasisi hiyo katika miaka 25 ya utendaji wake tangu Juni 1997, imetoa elimu kwa wanufaika zaidi ya 6,000 ambao wamewafikia wanawake wengine zaidi ya 25,000 waliozalisha bidhaa zenye thamani ya sh. trilioni 11.
“Pamoja na bidhaa hizo, kumekuwa na bidhaa nyingine zenye thamani ya sh. bilioni 694 zilizoagizwa maalumu kwa soko la ndani na nje ya nchi katika vipindi tofauti tofauti,” alisema.
Alisema kuwawezesha uhitaji na fursa ya elimu katika ngazi mbalimbali ndani na nje ya nchi, wamesomesha wanufaika 1,755 kujenga shule, visima vya maji safi, matundu ya vyoo, madawati na kugawa viti mwendo kwa wenye ulemavu.
Katika upande wa afya, alisema walifanikiwa kujenga kituo cha kulelea watoto yatima wilayani Kibaha, mkoani Pwani, chenye miundombinu ya afya na miradi mbalimbali ya kilimo na uvuvi inayosaidia kuendesha kituo hicho.
Mama Mkapa alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia, kwa kazi kubwa aliyoifanya kuitambulisha filamu ya Royal Tour duniani, hivyo kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi mahususi kwa bidhaa na huduma za wajasiriamali nchini.
Na WILLIAM SHECHAMBO