WATANZANIA zaidi ya 300 wanatarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Desemba 5 hadi 9, mwaka huu katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, aliyasema hayo jijini Arusha na kuongeza kuwa Wizara yake imepanga kusherehekea miaka hiyo kwa njia ya kipekee katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kuonyesha uzalendo wa nchi.
“Upandaji huu wa mlima Kilimanjaro katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru, utakuwa ni mahsusi na wa kipekee kwa kuwa kutakuwa na makundi ya watu mbalimbali, ambapo nami nitashiriki,” alisema.
Dk. Ndumbaro alisema mpaka sasa watu zaidi ya 120 wameshajisajili kupanda mlima na kubainisha kwamba hamasa ni kubwa ya watu wanaotaka kupanda milima huo wa kipekee katika maadhimisho hayo.
Alitaja makundi ambayo yameshajisajili ni wabunge, wasanii wa kada mbalimbali, wana michezo, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa vyama vya siasa.
“Hamasa ni kubwa ya watu wanaojitokeza kujiandikisha kupanda mlima huo kupitia kampuni ya ZARA TOURS, inayomilikiwa na mzawa mwanamke Zainab Ansell, ambayo inashirikiana na serikali katika kuandhimisha miaka 60 ya Uhuru,” alisema.
Dk. Ndumbaro alisema idadi kubwa itakuwa ni vijana na lengo ni kuwafundisha uzalendo wa nchi na kutambua kuwa Mlima Kilimanjaro upo nchini Tanzania na kutumia fursa hiyo kuutangaza kikamilifu ndani na nje ya nchi.
“Watanzania wenzangu msikose fursa hii adhimu. Gharama ya kupanda mlima huo ni shilingi 800,000 kwa mtu mmoja, hivyo nitoe rai kwa Watanzania hususan vijana kutumia fursa hiyo kwa kuwa mlima upo katika bara la Afrika na nchini ili kuutangaza, lakini pia kuonyesha uzalendo kwa nchi yetu.”
Aliongeza kuwa: “Mlima Kilimajaro ni alama kubwa ya upendo. Tuupiganie na ndiyo sababu mwaka 1961 Luteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Alex Nyirenda, alipandisha katika mlima huo, mwenge wa Uhuru na bendera ya Tanzania ili kuonyesha ishara ya upendo, pasipo na upendo, amani pasipo na amani na matumaini pasipo na tumaini.”
Msanii wa vichekesho, Maxwell Machange ‘Mzee Shayo’ ambaye ni balozi wa kuhamasisha Watanzania kujitokeza kupanda mlima Kilimajaro, alisema atahamasisha watu mbalimbali kupanda mlima huo kwa kuwa ni kitu cha aibu Wazungu kuupanda, wakati mtu yupo Marangu Mtoni, hajawahi kufanya.
“Nitafanya kampeni za kijiji kwa kijiji katika kuhamasisha Watanzania kupanda mlima Kilimanjaro na kikubwa zaidi ni kuonyesha uzalendo. Pia tunataka dunia ijue kuwa mlima huu upo Tanzania na haupo katika nchi nyingine yoyote ile kama watu mbalimbali wanavyofanya kwa maslahi yao binfasi,” alisema.
NA LILIAN JOEL, Arusha



























