TANZANIA wiki hii inafanya kumbukizi ya miaka 22 tangu kufariki aliyekuwa Rais wa Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika kuelekea kilele cha siku ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kimeandaa kongamano maalum la kumkumbuka Mwalimu Nyerere, tarehe 12. 10. 2021, katika kampasi ya kivukoni, Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo lenye mada isemayo; Maono ya Mwalimu Nyerere katika Uongozi, Maadii, Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Jamii, alikuwa ni Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Joseph Sinde Warioba.
Mada mahsusi mbili ziliwasilishwa na baadaye kuchangiwa na wahudhuriaji. Mada ya kwanza; Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kudumisha amani na umoja kwa maendeleo ya jamii, iliwasilishwa na Makamu Mwenye wa CCM, Tanzania Bara, ndugu Philip Mangula.
Mada ya pili, Falsafa ya Mwalimu Nyerere juu ya Uongozi, na dhamira ya kweli katika kukuza uchumi wa nchi kwa maendeleo ya jamii, iliwasilishwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, ndugu Joseph Butiku.
Awali, kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Stephen Wasira, amemueleza Mwalimu Nyerere kuwa aliwaandaa Watanganyika kujitawala na kuondoa ubaguzi wa aina zote.
“Mwalimu Nyerere hakuwaibia Watanzania, mpaka kufa kwake, alikuwa ni Kiongozi aliyestaafu akiwa hana fedha ndani wala nje ya nchi,” anahitimisha Wasira.
Waongeaji wengine na jinsi walivyomuelezea Mwalimu Nyerere ni;
“Mwalimu aliitumikia nchi hii, hakuiibia. Alikataa kuitwa Mtukufu, alikataa kuitwa Mheshimiwa, wote tulikuwa ni ‘ndugu,” Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba.
Äliwaunganisha Watanganyika katika kukataa kutawaliwa. Alijenga misingi na mifumo ya kukutana, alikuwa muumini wa vikao na maamuzi ya pamoja. Aliamini umoja hujengwa na vikao kupitia majadiliano ya wazi na maelewano,” Philip Mangula.
Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu kama sisi, lakini alitambua mambo mawili yanayomweleza; Mosi; mtuo na Utu – Kwamba utu wa mtu utambuliwe na uheshimiwe, awe huru, ashiriki, aseme, aishi maisha bora. Pili; Je, huyu mtu anajihudumia kwa utaratibu upi kuanzia katika ngazi ya familia?”Joseph Butiku.
Kilele cha kumbukizi ya miaka 22 bila Mwalimu Nyerere, kitaifa, itafanyika terehe 14 Oktoba, 2021 Chato, Mkoani Geita.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, ambaoyo yatajumuisha sherehe ya kuzima Mwenge, atakuwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amirijeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan.



























