WATU watatu wamekamatwa wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wakidaiwa kuvamia makaburi ya wilayani humo, kubomoa na kuiba.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, aliyasema hayo na kubainisha kuwa watu hao walikamatwa baada ya kuvamia makaburi na kuiba vyuma (nondo na misalaba) na kwenda kuviuza ili kujipatia kipato.
“Baadhi ya watu wamekamtwa baada ya kuvamia makaburi ya wilaya yetu na kuiba nondo na vitu vingine na kwenda kuviuza kama chuma chakavu ili kujinufaisha na kujipatia kipato. Tabia hiyo jamii ya Kitanzania hatukuzaliwa nayo na siyo utamaduni wetu,” alisema.
Kalli amesema watu wanapaswa kutanguliza uzalendo kwa kuwa katika makaburi hayo wamesitiriwa waliotangulia mbele za haki, hivyo yatalindwa na kuheshimiwa na hawatakubali uharibifu mwingine utokee.
“Tunaendelea kuwasaka wengine na hawa tunaowashikilia lazima wafikishwe katika mkono wa sheria, liwe funzo kwa wengine wenye tabia hiyo ya wizi uliopitiliza na kukosa utu.”
“Mwenye akili hawezi kuiba nondo makaburini na kwenda kuuza chuma chakavu ili kujipatia fedha. Huo ni wendawazimu ambao haupaswi kufumbiwa macho na jamii,” alisema.
Mkuu wa Wilaya huyo alionyesha kukerwa, kusikitishwa na vitendo na tabia hiyo isiyo na chembe ya utu kwa baadhi ya watu kuvunja makaburi na kuiba vitu.
Amesisitiza hatakuwa na huruma kwa wahusika wa tuhuma hizo kwa kuwa si jambo la uungwana kwenda kuwabughudhi waliopumzishwa makaburini kwa kuyavunja, kuyafukua na kuiba vyuma, kisha kuyaacha wazi.
Juzi, Kalli aliwaongoza mamia ya wananchi wakiwemo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali kufanya usafi katika makaburi hayo ikiwa ni madhimisho ya siku ya usafi mkoani Mwanza.
NA BALTAZAR, MASHAKA,Magu





























