FARAJA kwa watoto yatima ni jambo linalochangia ustawi wa jamii, kuleta furaha na kuondoa upweke, ndivyo Kampuni ya JX Limited, inavyofanya kila ifikapo Desemba ya kila mwaka na imetoa msaada kwa watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Ijango, Sinza Madukani, jijini Dar es Salaam.
Leo Desemba 15, 2021, kampuni hiyo ya JX Limited imetoa msaada wa vyakula na mahitaji mbalimbali, yakiwemo ya mchele, unga, sukari, chumvi na sabuni vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 2.3, katika kituo hicho cha kulelea watoto yatima cha Ijango.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Juma Gurumo, amesema kampuni hiyo imejiwekea utaratibu wa kila mwaka mwezi Desemba kutumia faida ndogo walioipata mwaka mzima kutoa msaada kwa watu wanaouhitaji.
Aidha, Gurumo amesema wametoa msaada huo kwa Watoto wenye uhitaji ili kuendelea kuinga mkono serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ili watoto hao nao waweze kusherehekea sikuku za Krismasi na mwaka mpya kama watoto wengine.
“Kwa niaba ya JX Limited tumetoa msaada huu kwa watoto wenye uhitaji ili kuiunga mkono serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan, ili watoto hawa waweze kufurahia sikuku za mwisho wa mwaka kama ambavyo Watoto wengine waliopo majumbani kwao watafurahia,” amesema Gurumo.
Kwa upande wake mlezi wa kituo hicho Zaidia Hassan, ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwakumbuka watoto hao na kutoa rai katika taasisi zingine ziweze kuiga mfano huo.
Zaidia amesema kituo hicho kina jumla ya watoto 123 wote wakipatiwa mahitaji yote muhimu.
Na Abdurahman Jumanne



























