Watu 7 wameripotiwa kufa na wengine 20 wakiripotiwa kunasa huku 49 wakipelekwa hospitalini baada ya paa la kanisa la Ciudad Madero la Santa Cruz kuanguka huko nchini Mexico.
Taarifa hiyo imetolewa na Polisi katika jimbo la pwani la Tamaulipas ambao wamesema, idadi ya watu 100 walikuwa kwenye misa wakati wa tukio la kuporomoka kwa kanisa likitokea.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa misa hiyo ilikuwa ni hafla ya ubatizo.
Watoto kadhaa wanaaminika kuwa miongoni mwa walionasa katika tukio hilo na juhudi za kuwaokoa zinaendelea.
Baadhi ya picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha jengo la kanisa likiwa magofu huku watu wakizingira vifusi, wakitafuta sana waliokuwa wamenasa ndani.
Askofu wa dayosisi ya Tampico, José Armando Álvarez Cano, alituma ujumbe kwa jamii kwenye mitandao ya kijamii akisema kuwa kazi inaendelea ya kuwatafuta walio chini ya vifusi.
Chanzo: BBC