WATU wenye ulemavu kisiwani Pemba, wamekumbushwa kuendelea kujikinga na Uviko-19, kutokana na kuwa bado ugonjwa huo upo visiwani hapa.
Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa ya Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar ZAPDD, Mkubwa Hamad Juma, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya kujadili athari za ugonjwa huo.
Alisema ugonjwa huo umekuwa ukiendelea kuathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo ni vyema kwa kundi hilo, kuendelea kujikinga.
Mkumbwa alisema kundi la watu wenye ulemavu, ni moja yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa, hivyo ni wajibu kuendelea kujikinga na kufuata kikamilifu maagizo ya watalaamu wa afya.
Alisema kutokana na hatari na athari ya ugonjwa huo, ZAPDD imeona ni vyema kutafuta mradi huo na kuwapa elimu wanachama na viongozi wa jumuiya mbalimbali za watu wenye ulemavu Zanzibar.
“Bado ugonjwa Korona upo hapa kwetu na duniani kote, hivyo sasa ni wajibu wetu sisi watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, kuendelea kuchukua hatua,’’ alisema.
Awali, Mratibu wa ZAPDD, Tawi la Pemba, Khalfan Amour Mohamed, alisema kundi hilo ni hatari zaidi kuambukizwa kutokana na kuchelewa kupata uwelewa na elimu ya kinga.
Alisema, elimu inayoendelea kutolewa inahitaji mbinu mbadala kwa kundi la watu wenye ulemavu, hivyo ni vyema kuhakikisha wanafuatilia elimu hiyo.
Hata hivyo amewataka viongozi wa matawi ya Jumuiya za watu wenye ulemavu na wazazi, kuendelea kutoa elimu hiyo kwa makundi mengine.
“Jumuia ya ZAPDD inapopata mradi hupenda kuwashirikisha na makundi mengine, mfano watu wenye ulemavu wa viungo, usikivu na viziwi kwa lengo la kuona elimu inasambaa,’’ alisema.



























