Na REHEMA MOHAMMED
WALIOKUWA wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania Letshego Limited, maarufu kwa jina la Faidika, wamefikishwa katika Mahakama Hakimu mkazi ya Kisutu kujibu shitaka la wizi wa sh. milioni 700.
Washitakiwa hao ni Elisha Tengeni , Donald Kwaya na Elisha Mboka, ambao wamesomewa shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Evodia Kyaruzi.
Akisoma shitaka hilo, wakili wa serikali Nguka Faraji amedai washitakiwa walitenda kosa hilo kati ya Januari mwaka 2016 hadi Septemba mwaka 2017.
Imedaiwa kwamba, washitakiwa hao waliiba sh. milioni 700 mali ya Kampuni ya Letshego Tanzania Limited (Faidika), fedha ambazo zilifika kwao kutokana na nafasi zao za uwajiri.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, wamekana ambapo upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambapo ilipangwa Juni 30 mwaka huu.
Washitakiwa wote wamepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, likiwemo kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakao wasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni 350.



























