WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassa katika madini, sekta hiyo imezidi kuimarika hivyo anawataka watendaji wawe chachu ya kuleta mabadiliko.
Amesisitiza haja ya wataalamu wa sekta ya madini, kutambua kuwa Watanzania wanawategemea, hivyo watangulize maslahi ya nchi katika utendaji wao.
Waziri Mkuu Majaliwa, alisema hayo jijini Dar es Salaam, katika utiaji saini makubaliano kati ya serikali na kampuni nne za uchimbaji madini ambapo alisisitiza kuwa, kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais Samia sekta hiyo imezidi kuimarika.
Alisema uongozi wa Rais Samia, muda mchache aliopo madarakani sekta hiyo, imeendelea kujipambanua na kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo, wakati na wakubwa.
“Wote tukiunganisha nguvu nchi hii itapata manufaa katika sekta ya madini, nikuhakikishie maelekezo uliyotoa sisi watendaji wako tunayachukua ili kuleta mafanikio katika sekta hii,” alisema Waziri Mkuu Mjaliwa wakati akitoa neon la shukran mbele ya Rais Samia.
Waziri Mkuu alisisitiza haja ya agizo la Rais Samia la kutoa fursa katika sekta hiyo ili kunufaisha jamii kwa kuwa nchi ina bahati ya madini, hivyo ni kushirikiana katika kutunza rasilimali ni kutengeneza fursa.
Alisema ni muhimu jitihada hizo kuungwa mkono na wataalamu wa sekta ya madini, kwakuwa Watanzania wanawategemea, hivyo watangulize maslahi ya nchi.
BITEKO
Waziri wa Madini Dotto Biteko, alisema tangu Rais Samia aingie madarakani, amewavutia wawekezaji wa madini na kuongeza makusanyo ambapo ndani ya miezi sita makusanyo kutokana na mauzo ya madini yamefikia sh. trilioni 4.740 kutoka sh. trilioni 8.19 kwa mwaka.
Alisema hatua hiyo, inawafanya kuamini lengo lilipo la kufikia makusanyo ya sh. Bilioni 600 kwa mwaka kutoka sh. Bilioni 580 litavukwa.
“Kingine kinachotupa ujasiri ziara ulizofanya za kuwaita wawekezaji wamesikia na kuja kwa wingi, ambapo kwa muda mfupi tumetoa leseni 20,277 na katika leseni hizo, za wachimbaji wadogo ni 11,574 wachimbaji wakubwa na wakati ni 65, huku leseni za utafiti zikifikia 476,” alisema.
Alisema sekta ya madini imeweka historia kwa kuingia mikataba minne mara moja ambayo uwekezaji wake ni zaidi ya sh. trilioni 1.750, yakiwa matokeo ya utendaji wa Rais Samia.
KABUDI
Kwa upande wake Waziri wa sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema waliodhani ‘tiara imekata kamba’ sasa wamejua kuwa Rais Samia, ameishika kamba sawasawa na safari inaendelea kwa kasi.
Alisema akiwa katika timu ya wataalamu walianza kwa kutunga sheria mbili mpya na kufanya marekebisho ya sheria ya madini iliyokwepo.
“Nikushukuru kwa kazi kubwa mliyotupa ambayo tuliifanya kimya kimya, kwa umakini mkubwa chini ya usimamizi wa Hayati Dk. John Kijazi (aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi) na kukamilisha kwa gharama ya sh. milioni 11, huku tukiwa hatulipwi posho ni kujitolea,” alisema.
Alisema sheria hizo zimeleta mageuzi na sura mpya katika kuhakikisha umiliki, ulinzi, usimamizi, utawala na matumizi ya utajiri wa rasilimali za nchi katika sekta ya madini.
Na MARIAM MZIWANDA



























