JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia wanawake wawili kwa tuhuma za kufanya biashara ya ngono kwa njia ya mitandao ya kijamii na wengine 25 kwa wizi wa mtandaoni.
Watuhumiwa hao wamekamatwa kupitia Timu Maalumu ya Kuzuia na Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni, kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema watuhumiwa hao 25 walikuwa wakisambaza jumbe kwa njia ya simu na kujifanya wakuu wa shule,waganga na mawakala wa ‘freemason’.
“Watuhumiwa hao wamekuwa wakijifanya wahudumu wa kampuni za simu, huwatumia watu jumbe mbalimbali kupitia namba tofauti za simu na kujifanya wanania ya kuwasaidia badala yake wanaishia kuwatapeli”alisema
Akifafanua kuhusu wanawake wanaofanya biashara ya ngono, Kamanda Muliro, amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakisambaza picha na video za utupu kupitia mitandao ya WhatsApp, Facebook, Tinder na Exotic tz.
Aidha, Kamanda Muliro, aliwataja watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na wizi wa mtandao ni Julius Mwabula(20)mkazi wa Ifakara Mkoani Morogoro na wenzake 22.
Pia, Kamanda Muliro aliwataja wanaotuhumiwa na biashara ya ngono ni Mary Samson Sibora (23)maarufu kama Asha Zungu Mkazi wa Sinza, na Zainabu Yahaya Omary (23) maarufu kama Official Manka, Mkazi wa Buguruni Jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao walikamatwa kupitia oparesheni iliyoanza Juni 18 hadi 26 mwaka huu.
Vilevile Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao wamehojiwa kwa kina na taratibu za kisheria zinakamilishwa ili wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo.
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria linatoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na uhalifu kwa njia ya mtandao na njia nyingine, serikali na vyombo vyake imejipanga kupambana na uhalifu wa aina yoyote” amesema
Kwamujibu wa Kamanda Muliro, watuhumiwa hao wamekatwa na vifaa mbalimbali ikiwemo kompyuta mpakato mbili, kompyuta ya mezani moja, simu za mkononi 28, flashi mbili, kadi za simu 50 na ‘modem’ ya mitandao yote moja.
Aidha, Kamanda Muliro ametoa rai kwa wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuwa waangalifu na vitendo vya utapeli.
Ameongezaa kuwa wananchi wachukue tahadahari wakati wa kutuma fedha au kufanya biashara kwa njia ya mtanadao, ili kuepuka kutapeliwa
“Watu waache kufanya biashara haramu mitandaoni kama vile kuuza miiili yao “aliongeza.
Na IRENE MWASOMOLA