WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amesema bendera ya Tanzania kupamba katika jengo maarufu duniani la Barj Khalifa katika Falme za Kiarabu, ni heshima aliyopewa Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kufanya ziara nchini humo.
Akizungumza na UHURU kwa njia ya simu akiwa mjini Amsterdam, Dk. Ndumbaro amesema kuwepo kwa bendera ya Tanzania katika jengo hilo ni sehemu ya kuitangaza nchi kimataifa.
“Unakumbuka tarehe 26 (Februari), Rais Samia alitembelea kule na alikutana na kuzungumza na Diaspora, ile bendera ilipandishwa pale kwa heshima yake,”alisema.
Hata hivyo, Dk. Ndumbaro amesema Rais Samia ni miongoni mwa Marais Watatu waliopata fursa ya kutembelea maonyesho hayo na kwamba, hiyo ni fursa muhimu iliyoibuka na neema lukuki.
Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, bendera hiyo katika jengo hilo refu duniani italeta tija ya kuitangaza nchi katika Falme za kiarabu na hatimaye kuvutia watalii.
“Watu wataangalia watauliza ile nini, wataambiwa ni bendera ya Tanzania, bila shaka watakuja katika banda la Tanzania kupata taarifa zaidi na watataka kuijua vyema Tanzania, huo ni mkakati wa kuwavuta,” amesema.
Ameongeza kwamba Tanzania ina soko kubwa la watalii kutoka Falme za Kiarabu hasa wa uwindaji, lakini ushiriki wake katika maonyesho ya DUBAI EXPO 2020 umelenga kuvutia wengi zaidi kwa kuwa nchini humo hawaishi waarabu pekee.
“Dubai hawaishi Waarabu pekee kule kuna watu wengi kutoka mataifa mbalimbali ni eneo la kimkakati,”alisema.
Na JUMA ISSIHAKA