SERIKALI imesisitiza kwamba minada yote ya mifugo inapaswa kusajiliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, huku ikitahadharisha kuwa isiyosajiliwa itafutwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, alipozungumza na wafanyabiashara wa mifugo mkoani humo.
Kwa mujibu wa Waziri Ndaki, kumejitokeza tabia ya kuanzishwa kwa minada mingi ya mifugo, bila ya kusajiliwa na wizara hiyo.
“Ifikapo Februari 20, mwakani, minada kama haijasajiliwa itafungiwa na kufutwa kwa mujibu wa sheria zilizoko za mifugo. Minada ya awali, ya upili na ya mipakani lazima isajiliwe na Wizara ya Mifugo na Uvuvi,” alisema.
Kutokana na hilo, aliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinasajili minada yao huku akisisitiza kama haijasajiliwa wapeleke maombi wizarani ili ikasajiliwe.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki alipiga marufuku uanzishwaji wa machinjio, minada na mabucha ‘bubu’ na kuiagiza Bodi ya Nyama kuwachukulia hatua za kisheria wanajihushisha na mambo hayo.
Ndaki alisema kumekuwa na uanzishwaji wa machinjio na mabucha kiholela bila kusajiliwa na wizara na taasisi zake na kusababisha kero.
“Utakuta machinjio yanakuwa bucha la nyama na hapo hapo unakuwa mnada, ifahamike kuwa nyama ikitoka machinjioni ipelekwe katika mabucha ikauzwe. Machinjio yasigeuke kuwa bucha wala yasiwe minada,” alisema.

Katika hatua nyingine, Ndaki alisema atawasiliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuona namna ya kupunguza tozo za usafirishaji wa mifugo kutoka katika Halmashauri.
Alisema wamepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ya mifugo na bidhaa zake kuwa wanatozwa tozo nyingi, hivyo wameomba wapunguziwe.
Ndaki alisema watakaa kupitia sheria zilizopo kuwapunguzia tozo ili kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara hao.
Aidha, alimuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo na taasisi zake kuwaondoa watu wa kati maarufu ‘galagaja’ katika minada kwa kuwa hawako kisheria.
Waziri huyo alisema watu hao wamekuwa wakiongeza gharama kubwa kwa wafanyabiashara wa mifugo, hivyo aliwasihi wafanyabiashara wanunue mifugo kwa wafugaji na siyo kwa galagaja.
Mfanyabiashara wa Mifugo, Elias Christopher, alidai tatizo linaanzia kwa usimamizi kwa viongozi kwa kutofuata sheria.
Christopher alisema nyama zinauzwa hovyo mitaani bila kufuata utaratibu na sheria zilizopo na kuwasababishia wakati mgumu wa kufanya biashara zao.
Mfanyabiashara mwingine, Shaban Magomba alisema, changamoto kubwa wanazokutana nazo ni Halmashauri kuwatoza ushuru zaidi ya mara mbili.
Na JUMANNE GUDE



























