Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakzi (WCF) kwenye Tamasha la pili la kitaifa la Utamaduni linaloendelea katika viwanja vya Stendi ya zamani mkoani Njombe.
WCF ni miongoni mwa Taasisi mbalimbali za serikali zinazoshiriki ili kutoa huduma kwa wananchi na wadau mbalimbali waliokusanyika kutoka mikoa mbalimbali nchini ikiwemo ile ya Nyanda za Juu Kusini.
Akiwa kwenye banda hilo, Mhe. Dkt. Chana, alipata fursa ya kupewa elimu ya Fidia kwa Wafanyakazi iliyokuwa ikitolewa na Afisa Madai Mwandamizi wa WCF, Bi. Asia Jingu.
Alijulishwa kuwa WCF inatoa fidia endapo mfanyakazi ataumia au kuugua kutokana na kazi na endapo atafariki basi wategemezi wake watalipwa fidia.
Pia alielezwa kuwa Mfuko uliundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263 marejeo ya mwaka 2015] na inahusu waajiri na waajiriwa wote kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara.
Aidha Mhe, Waziri ambaye alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Nkombe ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa alielezwa kuwa Mfuko unatoa jumla ya Mafao saba ambayo ni pamoja na Huduma ya matibabu, Malipo ya ulemavu wa muda, Malipo ya ulemavu wa kudumu, Malipo kwa anayemhudumia mgonjwa, Huduma za utengemao, Msaada wa mazishi na Malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.
Tamasha hilo la Kitaifa linalofanyika mkoani humo linaongozwa na kaulimbiu inayosema “Utamaduni ni Msingi wa maadili tuulinde na kuuendeleza”.
CC: K-VIS BLOG, NJOMBE