Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dk. Pindi Chana amefungua Tamasha la pili la kitaifa la Utamaduni Agosti 25, 2023 katika viwanja vya Stendi ya zamani mkoani Njombe.
Katika Tamasha hilo wananchi wa Mkoa wa Njombe wameendelea kupata burudani na fursa ya kuuza na kuonesha bidhaa zao, huku mikoa mbalimbali iliyohudhuria tamasha hilo kupitia vikundi na Sanaa na ngoma vikionesha Utamaduni na kuuza kazi zao za ubunifu.
Akifungua Tamasha hilo Waziri Mhe. Pindi Chana amesema tamasha hilo ni utekekezaji wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambayo inatoa fursa kwa jamii kuenzi na kulinda mila na desturi pamoja na kuzirithisha kwa vizazi cha sasa na vijavyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa amesema Tamasha hilo limetoa fursa kwa wananchi wa Njombe hatua inayowaongezea kipato katika biashara zao, kuona utamaduni wa mikoa mingine pamoja na kuonesha kuonesha utamaduni wao.
Awali akitoa maelezo juu ya tamasha hilo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesema tamasha hilo ni utekekezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa Septemba mwaka 2021 mkoani Mwanza, lengo likiwa ni kurithisha Utamaduni, mila na desturi za makabila yote Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kutangaza Utamaduni wa Mtanzania.
Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema Tamasha hilo linajumuisha mashindano ya ngoma za asili, vyakula, maonesho ya flamu ikiwemo za Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika, kuitangaza Royal Tour, Mada mbalimbali kuhusu maadili na utamaduni pamoja na huduma ya upimaji wa afya na elimu ya lishe, uchangiaji wa damu pamoja na kuwepo kwa mechi za kirafiki na matembezi mafupi.