WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, amesema Rais Samia Suluhu Hassan haridhishwi na hali ya usawa wa jinsia iliyopo hususan katika ngazi ya uamuzi kuwa na idadi ndogo ya wanawake.
Amesema mwaka 2019 waliofikia nafasi ya uamuzi katika sekta ya umma wanaume walikuwa asilimia 74 na wanawake asilimia 26, hivyo Rais Samia amemtuma kuhakikisha kunakuwa na mpango wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika kuwaandaa, kuwawezesha kujitambua, kujiamini, kuwajengea uwezo na utayari wanawake kushika nafasi za juu za uongozi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, wakati wa mafunzo maalumu ya wanawake katika uongozi yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Waziri Jenista alisema idadi ya watumishi wa umma waliofikia ngazi ya uamuzi haimridhishi Rais Samia.
“Ni lazima kuhakikisha tunafika lengo la usawa wa jinsia, hasa katika ngazi ya maamuzi, idadi ya watumishi wa umma wanawake ni wengi kuliko wanaume, lakini kufikia nafasi za juu za uongozi wanaume ndio wengi hii haiwezekani kuna sehemu tuliteleza tusahihishe pamoja,” alisema.
Amesema Rais Samia amemtuma kuhakikisha ongezeko la wanawake katika uongozi wa juu wa taasisi na sehemu za kazi linakuwa suala lililo katika mipango ya kitaifa, kikanda na kimataifa na ishirikishe mkakati maalumu wa kuwaandaa, kuwawezesha kujitambua, kujiamini na utayari katika uongozi.
“Jana nilikuwa na Rais Zanzibar nimepata muda wa kuzungumza naye sana, amenituma nije hapa niwaambie kuwa Rais wetu anataka kuona wanawake tunakuwa na kiherehere cha uongozi na hili litafanikiwa kwa kujiamini na mimi namuahidi nitatekeleza hivyo, sisi wenyewe tuwe tayari kwa kuibua wanawake wenye uwezo ili watumikie taifa,” alisema.
Waziri Jenista amebainisha suala la kuwajengea uwezo wanawake katika uongozi liwe ajenda ya serikali na sekta binafsi, kwa sababu wapo wengi wenye uwezo katika utendaji, waaminifu na wakipewa nafasi wana moyo wa kujituma ipasavyo.
Amesema ni muda mwafaka wanawake kujiandaa katika uongozi kwa sababu yupo mwalimu mwenye uthubutu, mbobezi, mwenye uwezo mkubwa ambaye amekuwa kivutio ndani na nje ya nchi, mcha Mungu, mzalendo na mwenye maono kwa taifa lake, wanayeweza kumuangalia kama kioo katika kufikia malengo.
“Sisi tulio karibu yake, tunaomsaidia tunamtambua ni mtaratibu asiye na pupa katika maamuzi, halali na namna ya ufanyaji kazi wa Rais Samia ni aibu hata kumwangusha amekuwa msaada wa kila mmoja wetu, wengi waliamini ni mwanamke hawezi, lakini amewashangaza,” alisema.
Waziri Jenista amefafanua, matamanio ya wanaume wengi ni kusaidia wanawake lakini hawapo tayari kuona wao wanasaidiwa na wanawake hali inayosababisha kujenga hofu ya maendeleo yao.
“Mimi niliingia bungeni nikiwa na umri mdogo na kipindi hicho wabunge wengi ni wanaume, nilikuwa naishi Vita hoteli, wote waliokuwa hapo ni wanaume nilikuwa najifungia ndani nikitoka bungeni sitoki hadi asubuhi, jioni nawasikia huko chini wanafurahi wanakunywa mimi najiona kama mnyonge, Mama Makinda (Spika wa Bunge mstaafu Anna Makinda) aliliona hilo kuwa sipo sawa, alinihamisha na kunitafutia nyumba, kila Jumamosi wakawa wananichukua yeye na mama Anna Abdallah na Balozi Salome Sijaona hawakuniacha.
“Walihakikisha wananijenga na mimi sikuwaangusha hadi sasa nasimama kwa ujasiri wanawake tunaweza, wakati mwingine tukubali kujifunza kwa wanaoweza zaidi yetu na tushikane mikono katika mafanikio,” alisema.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, amesema wanaamini maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila kuwapo uongozi thabiti unaozingatia jinsia.
NA MARIAM MZIWANDA