Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki, (Mb), leo tarehe 18 Oktoba, 2023 ameongoza Mkutano Mkuu wa 25 wa UNWTO unaoendelea Jijini Samarkand, Uzbekistani.
Hatua hiyo imefuatia kuthibitishwa kwa Tanzania na Nchi Wanachama kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano huo.
Akiongoza Mkutano Mkuu wa UNWTO Mhe. Kairuki amezishukuru nchi wanachama wa UNWTO kwa kuichagua nchi ya Tanzania katika nafasi ya Makamu wa Rais na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na nchi hizo ili kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii duniani.
Alisema Tanzania itaendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Utalii katika mipango yake ya kukuza uchumi, kutoa ajira na kuchochea maendeleo ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, uzalishaji ajira na kuchochea maendeleo.
Aidha, Mhe. Kairuki ametoa rai kwa nchi wanachama wa Shirika la UNWTO kushirikiana katika kuinua Sekta ya Utalii kwa maendeleo ya wananchi.
“Tuungane sote kwa pamoja ili kuiinua zaidi sekta yetu ya utalii kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wetu” Mhe. Kairuki amefafanua.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alipendekeza kuanzishwa kwa Baraza au Jukwaa ambalo litakalojumuisha baadhi ya waandishi wa habari, Watu Maarufu wenye ushawishi katika kijamii, waandishi wabobezi wa habari za mtandao za utalii (travel bloggers)na wengine kwa lengo la kutangaza na kukuza utalii duniani kote.
Mkutano huo unaoendelea nchini Uzbekistani ulifungulia tarehe 16 Oktoba, 2023 na Rais wa Uzbekistan, Mheshimiwa Shavkat Mirziyoyev na unahudhuriwa na Mawaziri wa Utalii kutoka Nchi wanachama wa UNWTO zaidi ya 121 pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Taasisi za kifedha na wadau kutoka sekta binafsi.