WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, amemkabidhi zawadi ya mfano wa meli mwanamuziki maarufu Duniani mwenye asili ya Lebanoni Maher Zain, kutoka nchini Sweden anayejulikana kwa Nyimbo za Kaswida, kama sehemu ya kuhamasisha utalii hapa nchini.
Waziri Mchengerwa, amemkabithi zawadi hiyo katika tamasha maalum la siku moja lililofanyika usiku wa Machi 12, 2022, kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa vyombo vya usafiri na kukuza kipato kwa walemavu wasio ona wanaolelewa katika kituo cha Watu Wenye Ulemavu wa Kuona ‘VIMDAT’ kilichoko Kisemvule jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mamia ya mashabiki wake waliofurika kuburidika na nyimbo zake kabla ya kuhitimisha tamasha hilo, mwanamuziki huyo maarufu wa kaswida duniani aliyevalia tisheti yenye maneno (Tanzania Unforgettable) amesema uwepo wake Tanzania ni jambo asiloweza kulisahau Maishani mwake kutokana na uzuri wa Tanzania na ukarimu wa watu wake.
“Naishukuru Serikali ya Tanzania na ninakupongeza Mheshimiwa Waziri kukuona hapa na wewe umekuja kuburudika na nyimbo zangu kweli Tanzania siyo ya kusahulika, ” alisema Maher.
Akizungumza kwa niaba ya waandaji wa tamasha hilo Mwenyekiti Msaidizi, Yousra Alnahd, amesema tamasha hilo lililopewa jina la Maher Zain in Tanzania pamoja na mapato ya tamasha hilo kulenga ununuzi wa vyombo vya usafiri kwa ajili ya kituo hicho, pia waandaji walilenga kutangaza utalii kama sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, katika kuitangaza Tanzania na vivutio vyake.
Na AMINA KASHEBA