Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amefurahishwa na utendaji kazi wa Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Geita, Mhandisi Jabiri Kayilla, pamoja na wasaidizi wake, Mameneja wa Wilaya na watumishi mbalimbali wa RUWASA Mkoa wa Geita katika utekelezaji wa miradi ya maji na kumuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kutoa motisha ya shilingi milioni 10 kwa utendaji kazi wao.
Waziri Aweso amefikia uamuzi huo mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Mbwanga uliopo wilayani Chato mkoani Geita.
Amesema ameshuhudia utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini lakini RUWASA Mkoa wa Geita chini ya mhandisi Jabiri Kayilla wanafanya kazi kubwa na kwa umaridadi zaidi katika kutekeleza miradi ya maji.
Waziri Aweso ametumia nafasi hiyo kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri kuhakikisha anawapa shilingi milioni 10 RUWASA Mkoa wa Geita ambayo itagawiwa kwa watumishi wote kama motisha ili kuongeza morali ya kazi huku akiwataka watumishi wengine wa mamlaka za maji nchini kuiga mfano mzuri unaofanywa na RUWASA Mkoa wa Geita.