Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Adolf Mkenda amewaaga wanafunzi 30 wa fani ya uhandisi ujenzi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ( DIT) kwenda masomoni nchini China kwa miaka miwili katika chuo cha uhandisi cha Chongqing (CQVIE).
Profesa Mkenda aliwaaga wanafunzi hao leo Dar e s Salaam na kuwataka kusoma kwa bidii na kuwa watu bora katika kuchangia maendeleo ya nchi.
Alisema program ya wanafunzi hao kwenda nchini China ni makubaliano yaliyoingiwa na serikali kupitia Taaasisi hiyo na Chuo hicho kilichoko China na kwamba wanafunzi hao watasoma kwa miaka miwili nchini humo na kurudi Tanzania kusoma kwa mwaka mmoja ili kuhitimisha shahada zao.
“Tayari wameshasoma mwaka mmoja katika chuo hicho na kufanya mafunzo kwa vitendo katika kiwanda cha Group Six International kwa miezi mitatu, hivyo kwa muundo wa mafunzo hayo watapata cheti cha diploma nchini China lakini shahada watamalizia DIT kwa mwaka mmoja ukijumuisha miaka minne,” alisema Profesa Mkenda na kuongeza kuwa udhamini wote wa wanafunzi hao umefanywa na China.
Alitoa wito kwa serikali ya China kuongeza udhamini kwa wanafunzi wote 300 wanaosajiliwa katika fani hiyo kwa mwaka ujao waweze kwenda kupata mafunzo nchini humo na kama haitowezekana ione namna ya kuangalia udhamini mbalimbali wanazotoa kwa Tanzania zipungue ili zielekezwe kwa wanafunzi hao ili kuleta mageuzi makubwa ya elimu nchini.
Alisema serikali itaandika andiko kwa wizara ya mambo ya nje kuona namna udhamini huo unavyoweza kunufaisha wanafunzi wengi nchini ikiwa ni kutimiza ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za kutaka mageuzi makubwa ya elimu hususani elimu ujuzi na vitendo kuongezeka.
Profesa Mkenda alisema kwa utaratibu huo pia wataangalia namna ya kupeleka wahadhiri ili kujifunza na kurudi ili kuimarisha uwezo nchini lakini pia kubadilishana wakufunzi ili kupata elimu kutoka China.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya DIT,Richard Masika alisema wanafunzi hao watasoma kwa mataala wa DIT kwa kuwa unawiana na unaotolewa katika chuo hicho.
Alisema DIT ilianza mchakato wa kufikia hatua ya wanafunzi hao kwenda China kwa kadhaa iliyopita ambapo walikuwa wakienda vijana wachache lakini kwa program hiyo nikuonesha kuwa wamevuka hatua kubwa.
Aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii, kuongeza ujuzi na ubunifu lakini pia wakionesha tabia njema na kuzingatia maadili ya watanzania.
Mwenyekiti wa viwanda vya GroupSix Intenational Sino Tanzania, Janson Huang alisema kutekelezwa kwa program ya kupeleka wanafunzi China ni hatua kubwa yenye mafanikio na maendeleo kwa nchi.
Alisema program hiyo itachangia ubunifu na kukua kwa maendeleo nchini.