WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile, amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kwa kushiriki maonyesho ya 45 ya sabasaba na bidhaa za ubunifu zinazojibu changamoto za maambukizi ya virusi vya corona.
Dk. Ndugulile ametoa pongezi hizo, katika banda la TTCL kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam alipotembelea kujionea bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL.
Amesema TTCL na Kituo cha Taifa cha Intaneti (NIDC), wamekuja na mfumo wa ukusanyaji wa fedha katika baadhi ya mageti na huduma kwa kutumia kadi za kitaifa za kutunzia fedha na kufanya miamala inayojulikana kama ‘N-Card’.
Waziri huyo ameongeza kuwa TTCL pia limeleta huduma ya kufanya mikutano kwa njia ya video ‘Video conference’ huduma ambayo inawawezesha watu kufanya mikutano yao bila kulundikana eneo moja, ambapo inajibu changamoto ya mikusanyiko hasa kipindi hiki cha tishio la ugonjwa hatari wa virusi vya corona.
Amesema matumizi ya ‘N-Card’ yanaondoa utaratibu wa awali wa malipo taslimu, hususan katika maeneo yenye misongano ya malipo kama katika viingilio uwanjani, baadhi ya mageti na hata kwenye matamasha, utaratibu ambao ni hatari hasa kipindi hiki ambacho mikusanyiko na misongamano isiyo ya lazima haitakiwi.
Kwa upande wake, Meneja wa Banda la TTCL, Ramadhani Mshana, akizungumza ndani ya banda lao, amezitaka taasisi binafsi na za umma zinazohitaji kupatiwa huduma za TTCL, kutembelea banda lao kupata utatuzi wa mahitaji yao.



























