Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amesema Wizara yake inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi nchini.
Waziri Silaa amesema hayo Desemba 22, 2023 jijini Dar es salaam wakati wa kikao chake na Wahariri wa vyombo vya Habari kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu siku 100 tangu alipoingia kuhudumo ofisi hiyo alipoteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Wizara inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini ambayo yanalenga kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi” amesema Waziri Silaa.
Miongoni mwa maboresho hayo ni Programu ya Kupanga, Kupima, Kumilikisha ardhi (KKK) kwa kushirikisha sekta binafsi na mamlaka za upangaji ambapo katika maboresho hayo yatafanyika marekebisho ya utaratibu wa kukopesha fedha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Viwanja utakaokuwa unatunza fedha na kukopesha fedha kwa ajili ya programu hiyo.
Aidha, amesema Wizara inakamilisha maboresho ya mfumo wa TEHAMA ambao utaruhusu huduma na miamala ya sekta kuanza kutolewa kidigitali na mfumo huo utaanza kutumika hivi karibuni kwa kuanza na mikoa ya Arusha, Tanga, Mwanza na Mbeya.
Ili kuendana na sayansi na teknolojia, Waziri Silaa amesema kuwa, Wizara hiyo imezindua rasmi mfumo wa ARDHI KLINIKI KIGANJANI maalumu kwa kupokea na kushughulikia malalamiko yatakayowasilishwa kwa kutumia simu ya kiganjani au kompyuta ili kuwahudumia watanzania kwa urahisi katika sekta ya ardhi.
Zaidi ya hayo Waziri Silaa amesema kuwa, Wizara ya Ardhi inafanya mabadiliko ya kimuundo na ya kiutendaji kwa kuanzisha mikoa maalumu ya ardhi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa na kwa kuanzia imeanza na Mkoa wa Dodoma na Dar es Salaam. Hata hivyo, amesema maboresho hayo yanaweza kuendelea kufanyika katika mikoa yenye miamala mingi ya ardhi ikiwemo Mkoa wa Mwanza na Pwani.