WIZARA ya Fedha na Mipango, imeidhinishiwa bajeti ya sh. trilioni 14.94 yenye vipaumbele nane ikiwemo mkakati wa serikali kupunguza uhaba wa mafuta ya kula na sukari nchini, ambapo imepanga kutoa mikopo ya sh. bilioni 78 kwa sekta ya viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo.
Pia, serikali imepanga kutoa mkopo sh. bilioni 130 kwa ajili ya ununuzi wa pamba na kahawa nchini.
Akizungumza Bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2022/23, waziri wa wizara hiyo, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema fedha hizo zitatolewa na serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
“Katika mwaka 2022/23, benki ya TADB imepanga kutoa mikopo ya sh. bilioni 78 kwa sekta ya viwanda, hususan viwanda vya mafuta ya kula na sukari katika mikoa ya Kigoma, Shinyanga na Manyara. Mikopo hiyo inatarajia kupunguza upungufu wa mafuta ya kula na sukari hapa nchini,” alisema.
Dk. Nchemba alisema ili kuchochea na kudhibiti ustawi wa viashiria vya uchumi jumla, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepanga katika mwaka 2022/23, kukuza wastani wa ukuaji ujazi wa fedha kuendana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Dk. Mwigulu, BoT imepanga kudhibiti na kupunguza kiwango cha mikopo ‘chechefu’ na kuweka akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Aidha, alieleza katika mwaka 2022/23, Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) imepanga kutoa mikopo ya sh. bilioni 47 kwa sekta ya viwanda, maji, nishati, madini, mafuta na gesi, huduma, utalii na kilimo.
MALIPO YA PENSHENI
Dk. Nchemba alisema hadi Aprili, mwaka huu, wizara imelipa mafao na pensheni kwa wastani wa wastaafu 59,825 kila mwezi, mirathi kwa warithi 1,038, malipo ya malezi kwa walezi 1,246 na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi 500 wa serikali walio katika mikataba.
“Wizara imeendelea kuboresha mfumo wa huduma ya pensheni, mirathi, utunzaji wa kumbukumbu,
uhakiki wa wastaafu, ulipaji mafao na pensheni kwa watumishi wa serikali ambao sio wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na mirathi na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi wa serikali walio katika mikataba na viongozi wa kisiasa,” alisisitiza.
Alisema wizara inaendelea kufanya uhakiki wa wastaafu wanaopata malipo ya pensheni kupitia Hazina.
UKUSANYAJI KODI
Dk. Nchemba alisema katika mwaka 2022/23, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kuhuisha mkakati wa muda wa kati na mrefu wa ukusanyaji mapato, kutunga upya sheria na kanuni za ushuru wa stempu na bidhaa.
Alieleza TRA inatarajia kuanzisha maabara ya forodha, kutengeneza na kutekeleza Mfumo Unganifu wa Kusimamia Mapato ya Ndani na kuboresha Kituo cha Udhibiti na Ufuatiliaji wa Mifumo.
“Taasisi za rufaa za kodi zitaendelea kusajili, kusikiliza na kutoa maamuzi ya maombi, mashauri na rufaa za kodi ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini,” alisema Dk. Nchemba.
TAASISI ZA BIMA
Waziri huyo alifafanua katika mwaka 2022/23 Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inatarajia kufanya uchambuzi wa mikataba ya bima kwa kampuni 30 za bima nchini.
Pia, alisema TIRA itakagua kampuni 30 za bima, madalali 70, benki wakala 26 na mawakala 278, kufanya upekuzi wa kina ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kampuni 10, kutoa elimu ya bima kwa watu milioni 1.5 kuhusu huduma za bima na kuhamasisha kampuni hizo kuandaa bidhaa za bima katika sekta ya kilimo.
Alisema Shirika la Taifa la Bima (NIC) linatarajia kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa huduma hiyo, kubuni bidhaa mpya nne za bima, kuhamasisha na kufuatilia uandikishaji wa bima kwa taasisi za umma 100 ambazo hazijakata bima kupitia NIC.
VIPAUMBELE VYA WIZARA
Waziri Dk. Mwigulu alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, wizara imepanga kukusanya, kutafuta na kudhibiti mapato na matumizi ya serikali na kuhudumia kwa wakati deni la serikali pindi linapoiva.
Pia, alisema wizara itafanya tathmini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ikiwa ni
maandalizi mahsusi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kufanya tathmini ya mfumo na muundo wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuwezesha kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo.
Vipaumbele vingine ni kurejesha Bahati Nasibu ya Taifa, kufanya tafiti katika sekta za uzalishaji ili kuibua fursa za uwekezaji, uwezeshaji na vyanzo vya mapato ya serikali katika muda mfupi, kati na mrefu.
Pia, alisema kuendelea kutekeleza maagizo ya serikali ya kutafsiri sheria za wizara na taasisi zake kwa lugha ya Kiswahili na kuhuisha Mwongozo wa Taifa wa Usimamizi wa Viashiria Hatarishi.
Kwa upande wa matumizi ya maendeleo, alisema wizara inatarajia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma Awamu ya Sita (PFMRP VI).
Dk. Mwigulu alieleza wizara inatarajia kuandaa na kujenga ghala la takwimu, kuratibu na kusimamia sensa ya watu na makazi na kuziwezesha taasisi za wizara, hususan za elimu na mafunzo kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia.
NA SELINA MATHEW Dodoma