Wizara ya Katiba na Sheria imeendesha Mafunzo kwa Waandishi wa Habari Waandamizi nchini Tanzania kuhusu Sheria na Kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi zenye lengo la kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu kwa kuwatambua na kuwalinda watoa taarifa na mashahidi.
Mafunzo hayo ya siku mbili (Oktoba 10 – 11,2023) yanafanyika Mkoani Morogoro yakikutanisha waandishi wa habari waandamizi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro, Neema Haule amesema Kanuni hizo zitasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka katika jamii inayowazunguka.
“Taarifa hizo za uhalifu zimekuwa zikitolewa na kupokelewa siyo tu kwenye vyombo vya dola bali kupitia vyombo vya habari na vyanzo vingine vilivyobainishwa katika sheria ya Ulinzi wa Watoa taarifa na Mashahidi ya Mwaka 2015 (The Whistleblower and Witness Protection Act, 2015). Kanuni hizi zitakuwa msaada sana kwani pamoja na masuala mengine zinaweka taratibu za kuwalipa au kuwapa fidia watoa taarifa na mashahidi kutokana na madhara yatakayowapata kutokana na ama taarifa walizotoa au kuhusika katika kutoa Ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu”,ameeleza Haule.
Amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa wanahabari waandamizi ili wawe mabalozi na kuihabarisha umma kuhusu taratibu za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi ambapo wataelimishwa kuhusu Sheria ya Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi Sura ya 446 na Kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi, Kanuni zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Namba 59 la tarehe 10, Februari 2023.
“Niwaombe kupitia taaluma yenu ya habari tuendelee kutoa elimu ya kisheria kwa umma wa Watanzania kuhusiana na sharia na kanuni hizi ili wawe na uelewa na wajue umuhimu wa kuwafichua wahalifu wa makossa mbalimbali yanayotendeka katika jamii yetu ili mwisho wa siku matukio ya kiuhalifu yaweze kupungua na kuisha kabisa”,amesema.
Amebainisha kuwa msisitizo mkubwa wa matumizi ya Sheria na Kanuni hizo ni kuhamasisha wananchi watoe taarifa kuhusu uhalifu unaotokea au unaotarajiwa kutokea katika jamii ambayo inatakiwa iwe sehemu salama ambayo kila mwananchi ataishi kwa amani na utulivu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Burton Mwasomola amesema lengo la Sheria na Kanuni hizo ni kufichua maovu katika jamii, makossa ya kiuhalifu ikiwemo ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa umma.
“Lengo ni kuhakikisha mashahidi wanalindwa kwa mujibu wa Sheria. Wote tuliowaita hapa majina yenu ni makubwa, nyinyi ni waandishi wa habari wanufaika wa mwanzo kabisa kwa sababu Sheria hii na kanuni hizi ni mpya kabisa”,amesema Mwasomola.
Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi, Ufuatiliaji na Tathmini Programu ya BSAAT, Ofisi ya Rais, Ikulu, Bw. Josiah Mathania amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaelisha waandishi kuhusu sharia na kanuni ili kuwalinda watoa taarifa na mashahidi.
“Tunaamini nyinyi waandishi wa habari waandamizi mtasaidia kuelimisha wananchi kuhusu kutoa taarifa. Sasa wananchi wataweza kutoa taarifa bila uoga na taarifa zitaongezeka. Hizi taarifa sasa zitatoka bila hofu kwa wananchi ambao awali walikuwa wanapata hofu kutoa taarifa”,amesema.
Akielezea kuhusu Programu ya Building Sustainable Ant Corruption Action in Tanzania (BSAAT), amesema ni Programu ya kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa nchini ambapo lengo kuu ni kuisaidia serikali ya Tanzania katika juhudi zake za kupambana na rushwa kwa kuziwezesha Taasisi 10 zinazolenga kupambana na rushwa nchini.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni TAKUKURU,Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Sekretariati ya Maadili ya viongozi,Ofisi ya Msajili wa Makampuni,Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu, Mahakama ya Tanzania, Idara ya Utawala Bora na Maboresho, Ikulu.
Ameongeza kuwa Programu hiyo inaratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu ikipata ufadhili kutoka Serikali ya Uingereza na Umoja wa nchi za ulaya (EU) ambapo kila mwaka kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 6 kwa mwaka zinatolewa kwa Taasisi hizo 10.
“Programu ya BSAAT inapimwa kwa viashiria vikuu vitatu ambavyo ni kuongeza taarifa shuku za rushwa, kupunguza muda wa kesi mahakamani na kurejesha/kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa”,ameeleza.
Ameongeza kuwa, Programu ya BSAAT ilifadhili Uandaaji wa Kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi pamoja na mafunzo kwa waandishi waandamizi wa vyombo vya habari.
“Programu inaamini kuwa baada ya mafunzo haya, wananchi watapata uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni hizi kupitia vyombo vyenu vya habari, na hivyo kupelekea kufanikisha kiashiria kikuu cha kwanza cha program ya BSAAT cha kuongeza taarifa shuku za rushwa/uhalifu”, amesema Mathania .
Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bi.Neema Haule akifungua Mafunzo kwa waandishi wa habari waandamizi kuhusu Sheria na Kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi yaliyofanyika leo Oktoba 10,2023 mkoani Morogoro.