Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuonesha ubabe wake kwenye mbio ambapo kwa upande wa wanaume imeibuka kinara kwenye mbio za mita 1500 na mshindi wa pili kwenye mbio za mita 400 huku kwa upande wa wanawake imeibuka mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 1500 katika Mashindano ya 37 ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea Mkoani Iringa .
Akizungumza leo mkoani humo mara baada ya ushindi huo Bw. Elibariki Buko ambaye ndiye mshindi wa mbio namba moja wa mita 1500 na namba mbili za mita 400, amesema ushindi huo ni matokeo ya uongozi makini wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii
” Ushindi huu sio wa kwangu mimi bali ni ushindi wa Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamekuwa msaada mkubwa kwetu kuanzia maandalizi hadi hatua hii. Niwashukuru sana Mimi pamoja na watumishi wenzangu kwa kuendelea kutuwezesha kushiriki katika michezo hii.
Ametumia fursa hiyo kuihakikishia Menejimenti ya Wizara hiyo kuwa yeye pamoja na wenzake watatumia michezo hiyo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini huku akiomba kuendelea kupewa nafasi zaidi katika kushiriki katika mashindano mengine ili waweze kukidhi ndoto na maono aliyonayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya utalii kitaifa na kimataifa.
‘’Tumeanza kutangaza utalii na vivutio vya utalii vilivyopo maeneo haya kama Hifadhi ya Ruaha na hata vivutio vingine kama Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.” amesema Buko.
Ameongeza,’’ imetusaidia pia kujenga ushirikiano na afya kwani nina uhakika mara tukaporudi katika maeneo yetu ya kazi umakini na uhodari katika kuhudumia watanzania utaongezeka’’
Kwa upande wake Jehovaness Sarakikye ambaye ndio mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 1500 kwa wanawake amesema, aliamini atashinda mbio hizo mara baada ya kufanya maandalizi ya kutosha huku akiwapongeza Walimu kwa kuwaandaa vzuri kwa ajili na shindano huo.
‘’Tulijiandaa vizuri, haikuwa rahisi lakini nawashukuru sana Walimu wetu walifanya kazi nzuri ya kutuandaa kwa ajili mchezo huu’’ Alisema Sarakikye.
Naye Mratibu wa Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Leodger Kiwia ametumia fursa hiyo kuwapongeza washindi hao kwa kuipatia ushindi Wizara huku akisisitiza kuwa Wizara itahakikisha inaendelea kupambana ili kushinda michezo iliyobakia na hatimaye kubeba vikombe vyote.
” Nawapongeza sana Washiriki wetu wote ikiwemo na hawa wa Riadha, ushindani ulikua mkali sana lakini hatimaye wameiletea Wizara yetu furaha. Sisi kama Viongozi tutaendelea kusaidia wachezaji hawa kwa namna yeyote ile ili watuletee ushindi na hatimaye tupeleke vikombe nyumbani’’ Amesema Kiwia