VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamezidi kukaa patamu baada ya kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wakifikisha pointi 19, katika mechi ya mzunguko wa saba.
Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza, katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Mbeya Kwanza ikiwa ndio msimu wake wa kwanza katika michuano hiyo, ilishindwa kuutumia uwanja wake wa nyumbani huku wakiwaacha Yanga kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa.
Mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku kila moja ikitaka bao la mapema ili kujiweka katika mazingira mazuri.
Bao la kwanza la Yanga liliwekwa kimiani na mchezaji Saido Ntibazonkiza katika dakika ya 18, kufuatia kupiga mpira wa faulo ilitokana na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuchezewa madhambi na beki wa Mbeya Kwanza nje kidogo ya eneo la hatari.
Wakitandaza kandanda safi huku wakigongeana pasi fupi fupi, Yanga walipata bao la pili kupitia kwa mshambuliaji Fiston Mayele katika dakika ya 26, baada ya kumalizia pasi murua iliyotolewa na Fei Toto na kuujaza mpira wavuni.
Dakika ya 33, Yanga nusura wapate bao jingine ambapo Fei Toto alifumua shuti lililoishia kwa kipa wa Mbeya Kwanza Hamadi Kadedi.
Hadi timu zinakwenda katika mapumziko, Yanga walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza Yanga wakionekana kulisakama lango la Mbeya Kwanza kwa kushtukiza, dakika ya 69, Djuma Shabani alikosa bao na shuti lake likatoka nje kidogo ya lango.
Mbeya Kwanza walijibu shambulizi hilo dakika ya 76 ambapo mshambuliaji wake Chrispin Ngushi alipata nafasi na kufumua shuti lililotoka nje ya lango.
Dakika tatu kabla mchezo kumalizika, Mbeya Kwanza walipata nafasi nyingine kupitia Hamis Kanduru, lakini hakuwa makini kukwamisha mpira wavuni.
Mbeya Kwanza: Hamad Kadedi, Miza Kristom, Brown Mwankemwa, Geofrey Raphael, Rolland Msonjo, Doglas Ambakisye, William Edger, Chesco Mwasimba, Oscar Mwajanga, Chrispin Ngushi na Hamis Kanduru.
Yanga: Djidgui Diara, Djuma Shabani, David Brayson, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke/Farid Musa, Zawadi Mauya, Fiston Mayele/ Haritie Makambo, Faisal Salum na Said Ntibazonkiza.
Na HERBON ADMIN, Mbeya