UNAWEZA kusema Yanga haipoi wala haiboi, baada ya jioni ya leo kutinga hatua ya Fainali ya Kombe la FA (ASFC), kufuatia kichapo cha bao 1-0, ilichokitoa kwa Biashara United ya Mara.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali kwa dakika zote 90,umepigwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Bao la ushindi la Yanga, limepachikwa wavuni na Yacouba Songne, katika dakika ya 22 ya mchezo, kwa shuti kali lililomshinda kipa James Sseba, baada ya kupewa pasi nzuri na Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inasubiri mshindi wa mchezo wa nusu fainali wa pili, kati ya Simba na Azam, utakaopigwa kesho, katika dimba la Majimaji mjini Songea.
Yanga walifika hatua hiyo baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga,katika mchezo wa robo fainali wakati Biashara United nayo ilifuzu hatua hiyo kwa ushindi kama huo dhidi ya Namungo FC.
Na MWANDISHI WETU