MKUU wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge, amesema tangu kuanza chanjo ya Uviko-19 mkoani Kagera, imepokea dozi 106,901, ambapo mpaka sasa wananchi 30,893 wamechanjwa.
Aliyasema hayo katika kikao maalumu cha ushauri cha mkoa huo na kufafanua kuwa mkoa ulipokea dozi hizo kwa awamu mbili.
Alisema awamu ya kwanza walipokea dozi 45,000, awamu ya pili walipokea 61,901 na kufanya jumla kuu kuwa 106,901, hivyo aliwashauri wananchi waendelee kujitokeza kupata chanjo hiyo.
“Viongozi wa ngazi zote tuendelee kuelimisha wananchi wetu faida za chanjo hii ili wajitokeze na kuchanja, kwani taifa lolote lenye kuwa na wananchi dhaifu, haliwezi kujenga uchumi imara,” alieleza.
Aidha, katika kikao hicho kilichojadili madhara na faida zinazoweza kujitokeza baada ya kumega Wilaya za Ngara na Biharamulo kwenda Chato, aliwaeleza kuwa yanapelekwa ngazi za juu kwa ajili ya maamuzi zaidi.
“Tulipata barua kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ya kututaka kupeleka mapendekezo yetu juu ya suala hilo, hivyo tumefuata taratibu zote za kupata mapendekezo kutoka Ngara na Biharamulo, Sekretarieti ya mkoa na wajumbe wa RCC wametoa mapendekezo yao ambayo yanapelekwa ngazi za juu,” alifafanua.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho, wakiwemo wabunge wa mkoa huu walionyesha wasiwasi wao kuwa wilaya hizo zikimegwa basi maendeleo na uchumi wa mkoa utashuka.
Mbunge wa viti maalumu (CCM) Bernadetha Mshashu, alisema wilaya hizo mbili ndizo zenye kubeba madini ya dhaabu na nikeli, Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato na vitega uchumi vingine muhimu.
Alieleza kuwa hali hiyo inaweza kusababisha mapato yatokanayo na fursa hizo kushuka, hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya mkoa huo.
Baadhi ya wajumbe kutoka Ngara na Biharamulo waliiomba serikali kuangalia kigezo cha upatikanaji kwa urahisi huduma za kijamii, ambapo walitoa mfano umbali wa kutoka Ngara kwenda Bukoba ni kilomita 320, wakati kwenda Chato ni kilomita 220.
Na Angela Sebastian, Bukoba



























