MWANAMITINDO wa mavazi nchini, Zara Bedel, amesema aliumia alipokosa nafasi ya kushiriki katika video ya wimbo wa Baira wa nyota wa muziki, Nassib Abdul ‘Diamond Plantinum’.
Akizungumza Dar es Salaam, Zara amesema sababu ya kukosa kuwepo katika video hiyo ni uwepo wa janga la ugonjwa wa corona.
“Ndoto yangu kubwa ilikuwa ni kufanyakazi na Diamond, lakini ugonjwa Uviko-19 ndiyo ulisababisha mimi kutokushiriki katika video hiyo,” amesema.
Zara ambaye alianza rasmi kazi ya mitindo mwaka 2018 kufanya shoo mbalimbali za mitindo hapa nchini na Afrika Kusini, amesema bado hajakata tamaa ya kufanya kazi na wasanii wakubwa ndani na nje ya nchi.
“Kazi zangu nyingi nafanya London nchini Uingereza, Sweden na Italia katika kampuni mbalimbali ambazo zinawahusisha wanamitindo,” alibainisha nyota huyo.
Aidha, Zara ametoa wito kwa wanamitindo nchini kuongeza juhudi katika kazi zao ili kufikia malengo.
Na AMINA KASHEBA