NA SOPHIA WAKATI, Handeni
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, amewataka wakuu wa Idara katika Halmashauri kuhakikisha wanaepuka kufanya kazi kwa mazoea, badala yake wazingatie kanuni, taratibu na sheria katika utendaji kazi.
Malima aliyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini, ambapo alisema uzoefu aliopata kutoka kwenye mabaraza ambayo amehudhuria tangu ateuliwe kuwa mkuu wa mkoa huo, amebaini kuwepo kwa ufanyaji kazi wa mazoea.
Alisema wakati umefika kwa watumishi wa halmashauri kubadilika katika kutoa huduma kwa wananchi hatua ambayo ina lengo la kuendana na kasi ya serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Malima alisema kubadilika kwa watumishi, kutachochea mabadiliko ya utoaji huduma na changamoto nyingi zitaondolewa, hivyo kupunguza kero za wananchi.
“Tangu nilipoanza ziara na kushiriki vikao vya mabaraza ya halmashauri ya Lushoto, Korogwe, Kilindi na Handeni, nimebaini baadhi ya upungufu huko nilikopita.
“Watumishi mnapaswa kubadilika ili kwenda na kasi ya serikali, mambo ya kujifanya miungu watu kwa kweli hayana nafasi kwa sasa,” alisema.
Mbali ya kutoa rai hiyo, Malima alisema kwa mtumishi ambaye hayupo tayari kubadilika, kamwe hatamvumilia kwa sababu serikali imelenga kuwaondolea kero wananchi.
“Hatua za kinidhamu hazitasita kuchukuliwa dhidi ya wale watakaoendelea kuzembea na kukataa mabadiliko, serikali inataka kutoa huduma bora kwa wananchi wake ili kuwarahisishia maendeleo yao,” alisema Malima.
Malima anaendelea na ziara ya kikazi katika halmashauri za mkoa wa Tanga zikiwemo Pangani, Muheza, Mkinga na Tanga ambapo katika baadhi ya maeneo aliyopita, amepata fursa ya kuhudhuria vikao vya mabaraza ya madiwani.





























