Na MARIAM MZIWANDA
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Davidi Silinde, amesema wizara hiyo imechukua hatua za haraka za kutafuta mwongozo wa usimamizi wa shughuli za machinga nchini, ili kudhibiti kero wanazokutana nazo ikiwemo matumizi ya mabavu yanayofanywa na baadhi ya mgambo.
Akizungumza na UhuruDigital, Silinde amesema hatua hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa hivi karibuni baada ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Sheilla Lukuba na kutaka kukomeshwa unyanyasaji wa aina yoyote ikiwemo matumizi ya nguvu yaliyopitiliza katika kuwaondoa machinga sehemu mbalimali.
“Baada ya agizo la Rais, wizara imeona kuna tatizo na tumechukua hatua ikiwemo kukutana na kitengo cha kushughulikia kero na matatizo ya machinga nchini, tumeagiza kikosi kazi hicho kutafuta mwongozo wa haraka ili kuwa na usimamizi mzuri wa shughuli za machinga, ikiwemo kudhibiti kero wanazokutana nazo za matumizi ya mabavu ya mgambo, baadae tutatoa tamko,” ameema.
Silinde amesema kikosi kazi kimeundwa na wizara hiyo ili kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo machinga.
Ameeleza kuwa, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho katika uteuzi na utenguzi, hivyo hatua zimechukuliwa baada kuagiza kusimamishwa kazi kwa viongozi hao kutokana na kukerwa na vitendo vya kunyanyaswa kwa machinga na kushindwa kuweka mpangilio mzuri wa maeneo ya kufanyia biashara zao.
Naibu Waziri Silinde, amesisitiza haja ya watendaji wa wizara hiyo kufanya kazi kwa umakini, uadilifu na kuwa sehemu ya kutatua kero za wananchi hususan wanyonge, ili kuisaidia serikali kuleta maendeleo.
Hatua hiyo imefikiwa, baada ya Rais Samia hivi karibuni akiwa katika ziara jijini Mwanza, alipokuwa akizungumza na vijana wa Tanzania kutangaza kutengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, katika wilaya hiyo wamachinga walitengewa eneo la mbali na mchanganyiko wa watu, hivyo waliamua kurejea maeneo ya awali kutokana na ugumu wa biashara.
Alimwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu kushughulikia changamoto ya wamachinga wilayani humo, huku akisisitiza kuwachukulia hatua viongozi watakaohusika kuwanyanyasa wananchi wanyonge.



























