Na FRED ALFRED, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amewataka wakuu wa wilaya mkoani hapa, kusimamia elimu, viwanda na kilimo ambavyo ni vipaumbele vya mkoa huo.
Mtaka ametoa agizo hilo wakati akizungumza baada ya kuwaapisha wakuu wa wilaya za Kondoa na Kongwa, ambao waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita.
“Ninyi ni wawakilishi wa Rais Samia ambaye amewaamini na kuwapa nafasi miongoni mwa wengi ambao wanahitaji nafasi hizo, sasa msilewe madaraka na kusahau majukumu yenu,” ameeleza.
Akaongeza kuwa: “Dodoma vipaumbele vyetu ni vitatu, lakini kikubwa katika elimu, tunataka tukafanye mapinduzi na ninyi ndio wawakilishi wa Rais hakikisheni katika wilaya zenu mnasimamia kikamilifu.”
Mtaka amesema Mkoa wa Dodoma bado uko chini katika sekta ya elimu, katika matokeo ya kitaifa hakuna shule za Dodoma katika shule bora 100.
Kuhusu ushirikiano, Mtaka amewataka wateule hao kujikita kusikiliza kero za wananchi na kujenga mahusiano baina ya ofisi ya mkuu wa wilaya na viongozi wa makundi mengine wakiwemo viongozi wa dini na Chama.
“Nawashauri msiwe na barehe ya madaraka, kuona ninyi mmeshakuwa matawi ya juu hamtaki kushirikiana na watu wengine, katika ulimwengu huu kila mtu ana umuhimu wake hakuna aliye juu zaidi ya mingine,” ameeleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remedius Emmanuel, amemshukuru Rais Samia kwa kumpa nafasi ya kumuamini kutekeleza kwa nguvu yale yote ambayo atatakiwa kutekeleza.
Amesema atahakikisha anashirikiana na watumishi wengine ili kuhakikisha analinda heshima na imani ya Rais aliyoionyesha kwake.
“Namshukuru Rais Samia kuniamini mimi kijana miongoni mwa vijana wengi kwa kunipa nafasi, nitailinda imani yake kwangu kwa kusimamia na kutekeleza yale yote ambayo yananipasa nitekeleze bila kuvunja sheria,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Khamis Mkadachi, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa, atashirikiana katika kuhakikisha anatekeleza adhima yake ya kuibadilisha Dodoma na kuifanya kuwa ya viwanda.
Amesema mipango ya kuifanya Dodoma ya viwanda itasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiilalamikia serikali kuwa hakuna ajira.
“Dodoma ni makao makuu ya nchi, lazima tuhakikishe tunashirikiana na mkuu wa mkoa kuhakikisha tunaboresha huduma zote za kijamii zikiwemo elimu, maji na kujenga viwanda kila wilaya ili kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wetu,” amesema.





























