Na IRENE MWASOMOLA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amepiga marufuku wafanyabiashara katika Soko la Machinga mkoani humo, ‘Machinga Complex’ kufungiwa biashara zao kwa kigezo cha kushindwa kulipa kodi.
Agizo hilo ni kati ya maagizo saba aliyoyatoa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, ili kuhakikisha soko hilo linatimiza lengo la kujengwa kwake ambalo ni kulihudumia kundi la wamachinga.
Makalla ameyasema hayo leo Juni 22, alipofanya ziara ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wamachinga wa sokoni hapo, huku akieleza kutoridhishwa na mazingira ya soko hilo.
Ameagiza pamoja na mambo mengine, kuwe na mpango mkakati wa kuendeleza soko hilo na kurejesha zaidi ya wafanyabiashara 3,000 waliotakiwa kuwepo sokoni hapo.
“Msifunge biashara za watu, sasa mtu mnamdai fedha alafu mnamfungia biashara mtazipataje fedha ? Msitoe tu hukumu muiteni halafu mwambieni wewe unadaiwa, mumpe mkakati wa kulipa deni , lazima kuwepo nakusikilizana, biashara zinachangamoto,” amesema.
Pia Makala amemuagiza meneja wa soko hilo, kuweka dawati maalumu la kusikiliza changamoto za machinga badala ya kukimbilia kufungia biashara zao.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ngwilabuzu Ludigija, kuweka mazingira rafiki kwa machinga sokoni hapo kwa sababu mazingira ya soko hilo hayaridhishi.
“Serikali imetumia fedha nyingi kujenga soko hili na mjadala juu ya soko hili naujua, upo udhaifu kwetu kwa kushindwa kuweka mazingira mazuri katika soko hili,” amesema.
Makalla amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Ilala Jumanne Shauri, kuhakikisha anashughulikia changamoto za maji, umeme na taka sokoni hapo kutokana na gharama kubwa za bili ya umeme.
Pia Makala aliutaka uongozi wa soko hilo kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri na masikilizano baina yao na wafanyabiashara waliopo sokoni hapo.





























