MKUU wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo, amesema barabara ya Taifa, inayopita pembeni mwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, itafungwa taa 32 za kisasa ili kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayojitokeza karibu na uwanja huo.
Jokate ametoa kauli hiyo leo, alipofanyika ziara katika eneo hilo ambalo lipo karibu na ofisi yake, baada ya kupata malalamiko ya wananchi kuhusu kuongezeka vitendo vya uhalifu vinavyofanyika katika barabara hiyo iliyopewa jina la Taifa (Taifa Road).
Katika ziara hiyo, mkuu huyo wa wilaya ameishukuru ofisi ya Manispaa ya Temeke, Mratibu wa mradi wa DMDP Temeke na Kamati ya Usalama kwa kukubali ombi lake la kuweka taa hizo za kisasa na bustari nzuri, katika maeneo hayo.
DC huyo amesema taarifa alizonazo, matukio mengi ya uhalifu hufanyika maeneo hayo baada ya kumalizika kwa mechi za jioni za mpira wa miguu au matamasha yanayohitimishwa usiku.
“Uwanja huu una taswira ya nchi yetu kimataifa kupitia michezo na dhifa mbalimbali za kitaifa, hivyo ni lazima hadhi ya eneo liendane na sifa hizi,” amesema.
Pia amesema eneo hilo ndipo ilipo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo nyakati za usiku huwa na giza linalochochea vitendo vya uhalifu.
Na Amina Kasheba



























