OFISI ya Rais imetengua maamuzi saba ya Tume ya Utumishi wa Umma na kukubali 52 yaliyokatiwa rufaa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya rufaa 153 za watumishi wa umma , kuwasilishwa kwa Rais na 59 kufanyiwa kazi ambapo kati ya hizo 52 zimekubaliwa na saba zimetenguliwa.
Aidha rufaa hizo ziliwasilishwa kwa Rais kutokana na watumishi hao kutokukubaliana na maamuzi yaliyotolewa na Tume.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Tume ya Utumishi wa Umma kutolea maamuzi mashauri ya watumishi 626 kwa mwaka 2019 hadi 2020.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa tume hiyo, Richard Cheyo, amesema wamehitimisha mkutano wa nne wa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo wamepokea na kutolea uamuzi rufaa 107 na malalamiko nane ya watumishi wa umma.
Cheyo amesema, katika miaka miwili hiyo tume imeshughulikia na kutoa maamuzi ya rufaa 626 kati ya hizo rufaa 219 zilikubaliwa, 227 zilikataliwa na 80 zilikatwa nje ya muda.
Aidha, warufani 153 walipinga uamuzi wa tume kwa Rais, ambapo ofisi yake ilifanyia kazi malalamiko hayo na kutolea uamuzi 59 ambapo rufani za watumishi 52 Rais amekubaliana na maamuzi ya tume na watumishi 7 amepinga na kutengua maamuzi ya tume hiyo.
“Pia rufani 94 bado zinafanyiwa kazi na Rais ndiye mamlaka ya mwisho ya uamuzi katika utumishi wa umma hivyo bila kutaja majina ya watumishi ambao rufani zao zimeamuliwa, tunasisitiza haja ya watumishi na waajiri, tunaiagiza mamlaka ya ajira na nidhamu kutekeleza majukumu yao ipasavyo,”amesema Richard Cheyo
Alitaja makosa ambayo yalisababisha rufani hizo kwa watumishi kuwa ni utoro kazini kwa siku zaidi ya tano bila ruhusa ya mwajiri, watumishi kwenda masomoni bila ruhusa, kutoa taarifa za uongo na kuajiriwa katika utumishi wa ummma bila sifa.
Mengine ni kughushi cheti cha uhitimu na kushindwa kuwasilisha cheti cha elimu ya kidato cha nne, kukosa uaminifu, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma na uzembe uliokithiri na kushindwa kutekeleza majukumu katika utumishi.
Amebainisha kuwa, ni muhimu mamlaka za ajira na nidhamu kutekeleza maagizo ya tume na kuwasilisha vielelezo vinavyohusiana na rufaa za malalamiko kwa wakati na kamati kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watumishi wa umma.
Cheyo ameeleza haja ya mamlaka hizo za nidhamu kuwa makini na uandishi wa hati za mashitaka na watumishi kujaza fomu za taarifa zao kwa usahihi na kuzingatia kanuni za maadili katika utumishi.
“Tume pia imejadili utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha kwa kuongozwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Dk. Steven Bwana,”Cheyo.
Ameongeza kuwa, katika kupokea na kutoa uamuzi wa rufaa hizo, tume ilijadili na kuamua rufaa 107 ambapo 76 zilikataliwa na tisa zilikubaliwa bila masharti na 12 kati yake zilikubaliwa kwa masharti kuwa mashauri yake yaanze upya kwa kuzingatia sheria.
Amesema pia rufaa 10 zilikatwa nje ya muda huku malalamiko yakiwa yamefanyiwa kazi ambapo matatu yalikataliwa na matano kukubaliwa.
Ametumia fursa hiyo kueleza taarifa ya robo mwaka Januari hadi Machi mwaka huu, ambapo wameshughulikia rufani 99 na malalamiko sita na kufanya ukaguzi wa masuala ya rasilimali watu katika utumishi wa umma.
Na MARIAM MZIWANDA





























