MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amewataka wasimamizi wa mradi wa kituo cha mabasi na malori cha Nyamuongolo, wakiwemo wataalamu wa halmashauri na mkandarasi, kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi huo, ulioko katika Halmashauri ya Ilemema, Mhandisi Gabriel amemtaka mkandarasi kufanya kazi mchana na usiku ili kumaliza mradi huo kwa wakati kulingana na muda wa mkataba.
“Mradi huu umecheleweshwa kulingana na mkataba wa awali, hivyo mhandisi wa mradi huu pamoja na mshauri nawataka kuandaa mpango kazi wenu mpya wa namna hii, kazi itakavyofanyika kwa wakati na kumalizika kwa muda muafaka,” amesema Gabriel.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iemela, kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki katika kila eneo linalojengwa katika mradi huo, ili utakapokamilika uwe mradi wenye tija kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Baada ya maelekezo hayo, Mhandisi Mshauri Mkazi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sylivesta Francis, amesema mradi huo ulianza kujengwa Julai 30, 2019 na ulitarajia kukamilika Machi 2021, lakini wamechelewa kutokana na changamoto mbalimbali.
Ameitaja sehemu ya changamoto kuwa ni pamoja na janga la ugonjwa wa Covid-19, ambapo iliwalazimu kupunguza wafanyakazi ili kujikinga na ugonjwa huo na uhaba wa saruji, hivyo sasa wanatarajia kukamilisha Septemba, mwaka huu.
Kituo hicho kitakapokamilika, kinatarajiwa kuwa na jengo la wamachinga kwa eneo la nje, ili kutoa fursa ya kiuchumi kwa wananchi, ambapo kinatarajiwa kugharimu sh. bilioni 28.
Na Johari Shani



























