UPO usemi maarufu katika lugha adhimu ya Kiswahili unenao, mwenye bahati kamwe hawezi kubahatisha.
Usemi huo umedhihirika kwa Mwanakijiji na mkulima wa mazao ya muhogo na nanasi mkoani Morogoro, kushinda na kukabidhiwa gari lenye thamani ya sh. milioni 169.
Abdallah Mohammed Mkazi wa Kinole mkoani Morogoro, ameshinda gari hiyo kupitia kampeni ya ‘Bonge la Mpango’ iliyokuwa ikiratibiwa na Benki ya NMB.
Akizungumza na UhuruOnline, Mkulima huyo amesema ushindi huo kwake ni kama ndoto za alinacha.
” Mimi ni Mkulima halafu ni Mwanakijiji, kwa hiyo ushindi huu umenipa funzo moja kubwa kwenye maisha yangu,” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Ukaguzi wa ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa, amesema kampeni hiyo imekuwa na dhamira ya kutambua mchango wa wateja wake.
Amesema wateja wa benki hiyo wamefanikisha NMB kuandika historia kwenye tasnia ya kibenki nchini, kwa kutengeneza faida ya sh. bilioni 206, kwa mwaka 2020.





























