KAMA kuna watu ambao watakuwa na kicheko basi ni mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam.
Pia, kama kuna watu ambao wanatembea kwa kuringa na kujisikia kutabasamu muda wote, ni hao hao mashabiki wa Yanga au ukipenda unaweza kuwaita Wananchi.
Hii inatokana na usajili mkubwa walioufanya kwa kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya 2021/2022 ambayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi mwezi ujao.
Yanga imetuliza akili, imeumiza kichwa kwa kufanya usajili wa kutisha ili kuhakikisha inafanya vizuri uwanjani haswa wakiwa na lengo la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wameukosa kwa miaka kadhaa mfululizo.
Leo litafanyika tamasha kubwa linalojulikana kwa jina la ‘Siku ya Mwananchi’, kuanzia saa 3:00 asubuhi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa kuanza na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.
Baadae utapigwa mchezo kati ya Yanga na timu ya Zanaco kutoka nchini Zambia.
WIKI ILIPOANZA
Ikumbukwe kuwa klabu ya Yanga ilianzishwa mwaka 1935, hii inakuwa mara ya pili kufanya tamasha kubwa kama hilo baada ya Agosti 30 mwaka jana kufanyika kwa mara ya kwanza na kufanya vizuri.
Tangu Jumatatu ya wiki hii, Yanga walikuwa na shughuli mbalimbali zinazoihusu klabu hiyo, ikiwemo kutambulisha jezi mpya, kutambulisha wasanii ambao watatumbuiza siku ya leo na leo ndio tamati ya yote waliyoyafanya kwa wiki nzima.
Yanga wakiwa katika maandalizi ya siku ya leo, huku wanachama, mashabiki wa timu hiyo wakitoa misaada mbalimbali nchi nzima na kusafisha Hospitali, makaburi nakufanya kazi mbalimbali katika maeneo yao wanayoishi.
Sambamba na hilo, wapenzi na wanachama wa Kanda ya Temeke Mkoani Dar es Salaam walikwenda Hospitali ya Temeke na kutoa misaada na kufanya usafi.
Huku tawi la Yanga Temeke Mikoroshini likifanya usafi katika Makaburi ya Nurul Imani Kata ya Sandali wakiwa na Diwani wa CCM,Christopher Kabalika.
WASANII KIBAO AKIWEMO KOFFI OLOMIDE
Katika tamasha la leo, uongozi wa Yanga umeeleza kuwa mwanamuziki mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR), Koffi Olomide ‘Mopao’, atakuwa mmoja wa wasanii ambao watatumbuiza.
Mopao ambaye ametua nchini jana mchana, anasema amekuja Dar es Salaam kusimamisha nchi, atafanya tamasha bora zaidi kwa kuwa hata yeye ni mpenzi wa timu hiyo ambayo ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara mara 27.
Wasanii wengine kadhaa ambao wameonesha utayari wa kujitokeza kwa wingi kusherehekea kwa pamoja na mashabiki wao ni Faustina Mfinanga ‘Nandy’ au ‘African Princess’, ametunga wimbo unaojulikana kwa jina la ‘Yanga’, ambao anatarajia kuutambulisha leo.
Wengine ambao watapamba tamasha hilo ni Billnas, Chege Chunga, Mheshimiwa Temba, Shishi Baby, Mzee wa Bwax, Juma Nature, Baba Levo, G Nako na wengine wataendelea kutambulishwa.
MECHI YA KIRAFIKI
Pia waliitangaza timu ya Zanaco kutoka Zambia, ndio watacheza nayo baada ya burudani kuisha na kuangalia soka kabambe kutoka kwa mastaa mbalimbali waliosajiliwa.
Jumatano iliyopita, pia walizindua jezi mpya kwa ajili ya msimu ujao ambazo mashabiki wamehimizwa kununua kwa wingi ili kuichangia timu yao.
Tukio lingine ambalo Yanga wamelifanya kwa wiki hii ni kumtambulisha, aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, kuhamia katika klabu hiyo kama msemaji pia hivyoakiwa kitengo kimoja na Hassan Bumbuli ambaye walikuwa wakitupiana maneno kipindi cha nyuma.
WATAMKUBALI MANARA?
Kutokana na uwezo wa kuongea na mashabiki aliokuwa nao Manara akiwa Simba, wanachama na mashabiki wa Yanga walimchukia lakini leo kahamia katika klabu yao, na utambulisho wake utafanyika pia leo katika tamasha hilo.

Kila mmoja leo ataondoka na jibu baada ya kutambulishwa Yanga, je mashabiki wamempokea Manara kuwa naye au wanamuona ni mpinzani wao kama ilivyokuwa awali, kwa kuwa aliwahi kusema hata wampe hela zote zilizopo benki kuu ya Tanzania, hawezi kuhamia Yanga.
Lakini sasa hivi amegeuka na kusema maneno yake sio msaafu wala biblia, yanaweza kubadilika muda wowote na wakati mwingine alikuwa anaongea vitu ambavyo hata yeye anaona haiwezekani kutokea.
MASTAA WATAKAVYO WASHA MOTO
Kuelekea tamasha hili, litakuwa maalum kwa kuwatambulisha mastaa wote wa Yanga ambao watacheza msimu wa 2021/2022.

Kabla ya kuanza kwa mchezo dhidi ya Zanaco FC, kutakuwa na utambulisho wa wachezaji wapya na wale wa zamani akiwemo Mghana Godfrey Nyalko, ambaye atatmbulishwa kwa mara ya kwanza.
Utambulisho huo utawakosa nyota wapya, mlinda mlango raia wa Mali, djigui Diarra na Mganda Khalid Aucho ambao wameitwa timu zao za taifa.
Wachezaji ambao watatambulishwa ni makipa; Ramadhan Kabwili na Erick Johara.
Walinzi ni Djuma Shaaban, Kibwana Shomari, David Bryson, Adeyum Saleh, Yassin Mustapha, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Yanick Bangala.
Viungo ni Mukoko Tumombe, Deus Kaseke, Feisal Salum ‘Feitoto’, Zawadi Mauya, Saido Ntibanzokinza, Farid Musa, Balama Mapinduzi, Jesus Moloko, Ditram Nchimbi na Dickson Ambundo.
Washambuliaji ni Fiston Mayele, Heritier Makambo, Yacouba Sogne na Yusuph Athumani.
Na ELIZABETH JOHN



























